Header Ads Widget

SHIRIKA LA TCRS KWA UFADHILI WA NCA LAWAPA MAFUNZO WAKULIMA WA ZAO LA NYANYA 20 WILAYA YA KISHAPU MKOANI SHINYANGA

 

Na Mapuli Kitina Misalaba

Shirika la Tanganyika Christian Refugee Service (TCRS) kwa ufadhili wa kifedha kutoka shirika la Norwegian Church Aid (NCA); limeendesha mafunzo yakuongeza thamani kwenye mazao hasa Nyanya, kwa wakulima pamoja na wadau wengine wa kilimo kutoka kata za Sekebugolo na Mondo Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga.

 Mafunzo hayo yamefanyika kwa siku tatu katika ukumbi wa mikutano kijiji cha Mwigumbi Wilaya ya Kishapu na kwamba yameandaliwa na shirika la TCRS huku wawezeshaji wakitoka  shirika la kuhudumia viwanda vidogo SIDO Mkoa wa Shinyanga.

Wakulima 20 walioshiriki mafunzo hayo wamepewa vyeti wakiwemo wafanyabiashara wa zao la Nyanya kutoka kwenye vijiji vinne ambavyo ni Mipa, Dulisi, Weshiteleja pamoja na kijiji cha Sekeididi na kwamba wamepewa mafunzo mbalimbali ikiwemo  usindikaji wa zao la nyanya ili kupata  Tomato Sauce and Tomato  Paste.

 Akizungumza kwenye mafunzo hayo afisa uendeshaji Biashara kutoka shirika la kuhudumia viwanda vidogo SIDO Mkoa wa Shinyanga Joseph Taban amewasisitiza washiriki baada ya kupata elimu hiyo, kujiendeleza zaidi na ujuzi huo ili waweze  kunufaika wao na jamii kwa ujumla.

“Baada ya mafunzo haya na leo hii tumetunukiwa vyeti yasiishie hapa hapa ni lazima tuhakikishe kwamba ujuzi huu tulioupata ukawe na manufaa kwetu na watu wengine wanaotuzunguka, hapa umepata ujuzi lakini ili uweze kuwa na manufaa, ujuzi huu ni wewe kuendelea kufanyia mazoezi hata kabla hujaanza kuanzisha hicho kiwanda kidogo cha usindikaji anza kusindika kwa ajili ya matumizi ya Nyumbani kwanza halafu badaye utakavyokuwa unafanya mara kwa mara utakuwa unagundua na vitu vingine ambavyo hukujifunza awali”.amesema Taban

 

Kwa upande wake afisa uendeshaji Biashara mwandamizi kutoka SIDO  Bwana Abel Bebwa amewasihi washiriki hao kujiamini zaidi kwenye utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo kuchangamkia fursa zinazojitokeza katika Maisha ya kila siku.

 Naye afisa Kilimo kutoka shirika la TCRS Wilaya ya Shinyanga Bwana Laurent Stanslaus amezungumzia umuhimu wa mafunzo hayo hasa kwa wakulima na wafanyabiashara wa zao la Nyanya.

“Mafunzo haya yanalenga hasa kuweza kupunguza matatizo ambayo yanatokana na uharibifu wa chakula kwa sababu kuna muda wakulima wanavuna mazao mengi hasa mazao yanayowahi kuharibika mfano zao la Nyanya akivuna halafu unakuta soko ni changamoto kwahiyo tumeona kwamba tuwape mafunzo haya ili mkulima aweze kuwa na uwezo wa kufaidika na mazao anayoyapata”.amesema Stanslaus

 Washiriki wa  mafunzo hayo wameshukuru TCRS, NCA pamoja na shirika la SIDO kwa kuwapa elimu hiyo ambayo wamesema itawasaidia kuinuka kiuchumi hasa katika Biashara pamoja na shughuli zingine za kwenye familia zao ikiwemo kusomesha watoto.

 

Afisa uendeshaji Biashara mwandamizi kutoka shirika la kuhudumia viwanda vidogo SIDO  Bwana Abel Bebwa akitoa maelekezo kwa washiriki wa mafunzo hayo kuhusu mambo muhimu ya kuzingatia katika usindikaji wa sosi ya Nyanya.



 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI