![]() |
Omari Singso Mwenyekiti wa kamati ya Hamasa ya timu ya Mashujaa ya Kigoma akizungumza kwenye mkutano wa kuinusuru timu |
Na Fadhili Abdallah, Kigoma
KLABU ya soka ya Mashujaa ya mkoani Kigoma inayoshiriki ligi kuu Tanzania Bara imetangaza kufanya mabadiliko ya uongozi ikiwa ni hatua ya kuinusuru timu hiyo kushuka daraja ikiwa inashirika nafasi ya 15 katika msimamo wa ligi kuu Tanzania Bara.
Mwenyekiti wa kamati ya hamasa ya timu ya Mashujaa Omari Singso alisema hayo katika kikao kilichohusisha uongozi wa timu hiyo, kamati ya hamasa na wapenzi wa timu hiyo kuzungumza kwa Pamoja mikakati ya kuinusuru timu hiyo kutoka mahali ilipo.
Singso alisema kuwa waliitwa na uongozi wa makao makuu ya jeshi na kuombwa kurudisha hamasa ya wananchi iliyokuwepo wakati wa kupandisha kutoka ligi ya Championship kuja ligi kuu zikiwa ni salamu kutoka kwa Mkuu wa Majeshi msafara ulioongozwa na Meja Jenerali Mbona.
![]() |
Meja Abdul Tika Mwenyekiti wa timu ya Mashujaa ya mkoani Kigoma ambaye amerudishwa kuinusuru timu isishuke daraja |
Mwenyekiti huyo wa Hamasa alisema kuwa wamepokea maombi hayo ya Mkuu wa Majeshi na kukubaliana kwa kauli moja kuibeba timu hiyo na ndiyo sababu ya kufanya mkutano huo ili wananchi na wapenzi wote watoe maoni yao ya nini kifanyike kunusuru timu baada ya wao kamati kuwasilisha maoni yao kwa uongozi huo wa jeshi.
Akizungumza kwenye mkutano huo Mwenyekiti wa timu ya Mashujaa Meja Abdul Tika ambaye amerudishwa tena kuiongoza timu hiyo baada ya timu kufanya vibaya na wapenzi kuisusa ikiwemo kutohudhuria mechi za timu hiyo kwenye uwanja wa Lake Tanganyika.
Alisema kuwa baada ya kupoteza mechi saba mfululizo na kuwa kwenye hatari ya kushuka daraja uongozi wa jeshi umekubaliana kwa kauli moja kubadilisha uongozi na yeye kurudishwa sambamba na kutafuta suluhu ya kuinusuru timu ikiwemo kuwarudisha wapenzi wa soka mkoani humo kuwa karibu na timu.
Sambamba na hilo Meja Tika alisema kuwa timu imewatimua idadi kubwa ya wachezaji wake kutokana na viwango duni, utovu wa nidhamu na tuhuma za usaliti (kuuza mechi) mambo ambayo yamesbabisha timu kupoteza mwelekeo na kukaribia kushuka daraja.
Kutokana na hilo alisema kuwa wameshaanza kufanya usajili wa wachezaji ambapo wachezaji watatu wameshatangazwa akiwemo Balama Mapinduzi (kipenseli), Ramadhani Mtumbuka na Mshambuliaji mmoja wa pembeni aliyefahamika kwa jina la Juma kutoka Inter Star ya Burundi.
![]() |
Wapenzi wa soka wa Mjini Kigoma waliohudhuria mechi ya kuinusuru Mashujaa isishuke daraja |
Aidha Pamoja na kurudishwa kwenye uongozi akiwa Mwenyekiti akichukua nafasi ya Meja Mgaya ambaye amepangiwa majukumu mengine alisema kuwa uongozi wa jeshi umemuondoa kwenye nafasi yake Afisa Habari wa timu hiyo Hamisi Miliango na nafasi hiyo itajazwa na mtu mwingine hivi karibuni akielezwa kuwa miongoni mwa viongozi waliozua taharuki baina ya uongozi wa timu na kamati ya hamasa na wananchi.
Baadhi ya wapenzi wa soka mkoa Kigoma waliopata nafasi ya kuzungumza kwenye mkutano huo akiwemo Salehe Nassoro maarufu Zahir alisema kuwa wameshangazwa kuona uongozi wa jeshi unaondoa viongozi waliopandisha timu, kuondoa idadi kubwa ya wachezaji na kutoshirikisha wananchi kwenye mipango mbalimbali ya kutafutia timu ushindi.
Nassoro alisema kuwa baada ya timu kupanda ligi kuu uongozi wa jeshi ulishindwa kufanya usajili wa maana na hivyo kuleta wachezaji wa kiwango cha chini ambao wameshindwa kuonyesha uwezo wao na kuifanya timu kufika hapo ilipo.
![]() |
Hanzuruni Kibera mmoja wa wapenzi wa soka Kigoma akitoa mchango wake wa mawazo kuinusuru mashujaa kushuka daraja |
Naye Hanzuruni Kibera alisema kuwa licha ya wachezaji kuwa na viwango vidogo vya kuweza kushindana wengi hawakuwa na nidhamu na walikuwa wakionekana kwenye mabaa wakizurula hovyo na wanawake hadi siku ya mechi.
Mwisho.
0 Comments