Header Ads Widget

MABORESHO BANDARI ZA ZIWA TANGANYIKA MOTO


Edward Mabula Meneja wa bandari za ziwa Tanganyika


Na Fadhili Abdallah, Kigoma

Uboreshaji mkubwa wa miundo mbinu na vitendea kazi katika bandari za ziwa Tanganyika unaelezwa kuongeza ufanisi mkubwa  katika upakiaji  na ushushaji wa shehena Kwenda na kutoka katika nchi za ukanda wa maziwa makuu.

Mkuu wa bandari za Ziwa Tanganyika, Edward Mabula akitoa taarifa kwa waandishi wa Habari waliokuwa wakifanya ziara kutembelea shughuli za utendaji wa bandari za mkoa Kigoma alisema kuwa bandari hizo zimetoa mchango mkubwa katika kusafirisha shehena Kwenda Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo  (DRC) zinazopitia bandari ya Dar es Salaam.

Mabula alisema kuwa uboreshaji huo umehusisha bandari 10 kati ya 19 zilizopo kwenye mwambao wa ziwa Tanganyika kwenye mikoa ya Kigoma,Katavi na Rukwa ambapo kiasi cha shilingi bilioni 108 zimetumika kufanya maboresho hayo ambayo yanahusisha uboreshaji wa maeneo ya kufanyia kazi sambamba na uwekezaji wa vifaa  vya kisasa.

Alisema kuwa katika hilo waliweza kununua mashine za kushusha na kupakia mizigo kwenye bandari za Karema winchi moja na bandari ya Kigoma winchi moja na Folk Lift sita.


Kutokana na hilo Mkuu huyo wa bandari za ziwa Tanganyika alisema mzigo umeongeza ambapo kwa  mwaka wa fedha 2022/2023 jumla ya tani 297,000 za mizigo zilisafirishwa na bandari hizo za ziwa Tanganyika Kwenda nchi za maziwa makuu na hasa Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo (DRC) na kati ya kiwango hicho tani 148,000 zilisafirishwa kupitia bandari ya Kigoma.                      

Metus Emanuel Mnongwa mmoja wa  wadau wanaotoa huduma ya kusafirisha shehena kupitia bandari ya Kigoma ameeleza kuwa kwa sasa hali ya utendaji kazi imeboreka ambapo shehena inachukua muda mfupi katika kushusha na kupakia ukilinganisha na kabla ya kuongezwa kwa vitendea kazi hivyo.

Naye Wakala wa ushuru wa forodha katika bandari ya Kigoma, Omari Zaidi alisema kuwa kwa miaka mingi vitendea kazi vilikuwa vikikwamisha upakiaji na ushushaji wa shehena kwenye bandari ya Kigoma lakini kwa sasa baada ya kuongezwa kwa vifaa hali imekuwa nzuri na changamoto kubwa imebaki katika upatikanaji wa mabehewa ya kutoka kutoka Dar es Salaam kuleta mzigo  Kigoma na mzigo kutoka Kigoma Kwenda Dar es Salaam.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI