Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Pamoja na kuwepo kwa utekelezaji wa mipango mbalimbali inayofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau imeelezwa kuwa kuwepo kwa huduma ya msindikizaji wa Mama Mjamzito kumechangia kupunguza vifo vya mama wajawazito na Watoto wakati wa kujifungua mkoani Kigoma.
Mhamasishaji jamii wa Shirika la Thamini Uhai, Ignus Kalongola alisema hayo wakati wa ziara ya kutembelea vituo vya utoaji huduma zinazotekeleza mpango huo na kusema kuwa hiyo ni moja ya hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali kwa kushirikiana na wadau katika kudhibiti vifo vya Mama Wajawazito na Watoto.
Kalongola alisema kuwa mpango unatekelezwa kwa Mama Mjamzito kuwa na msindikizaji tangu anapoanza Kwenda kliniki hadi siku ya kujifungua ambapo Msindikizaji huyo anaruhusiwa kuwepo karibu na mama Mjamzito hadi wakati wa kujifungua.
“Jambo hilo limeleta matokeo chanya kwani watu wengi wakiwemo wenza wa mama Wajawazito walitamani kuwa na watu kwa karibu kuwasaidia kwa namna yeyote lakini hapo awali haikuwa rahisi lakini kwa sasa imwezekana na imetoa hamasa kubwa kwa jamii hata kutumia vituo rasmi kwa ajili ya Kwenda kujifungua,”Alisema Kilongola.
Joseph Jackson ni mmoja wa wasindikizaji kwa mwenzake wake ambaye anasema kuwa amehamasika kumsindikiza mke wake tangu alipoanza kliniki ya ujauzito hadi kujifungua na sasa wanaongozana pia kliniki ya mtoto ili aweze kufuatilia kwa karibu maendeleo ya afya ya mke wake na mtoto.
Msindikizai huyo alisema kuwa mpango huo umemuwezesha kujua mambo mengi kuhusiana na masuala ya afya ya uzazi na anaweza kumsaidia mama mjamzito mahali popote ni jambo zuri ambapo anaomba wanaume wengi kulifuata.
Tecla Masanja ni Muuguzi wa kituo cha afya Kiganamo Halmashauri ya mji Kasulu alisema kuwa kwa sasa kumekuwa na ongezeko kubwa la mama wajawazito wanaofika kujifungua na ongezeko hilo pia limechangiwa na kuwepo kwa mpango wa Mama Wajawazito kuongozana na msindikizaji wake.
Kwa sasa kituo hicho kinazalisha hadi mama wajawazito 500 kwa mwezi kuanzi mwaka 2019 ukilinganisha na wastani wa mama wajawazito 200 waliokuwa wakijifungua wakati huo.









0 Comments