NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
SERIKALI imetoa misaada ya vyakula, magodoro, ndoo, madumu na mablangeti kwa kaya 119 za kata 8 za halmashauri ya Moshi mkoani Kilimanjaro zilizokumbwa na mafuriko.
Akikabidhi misaada hiyo, Naibu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga amesema kuwa, serikali inatambua shida iliyowakumba wananchi hao kutokana na mvua zilizonyesha na kupelekea mafuriko.
Alisema kuwa, mafuriko hayo pia yamepelekea vifo vya watu hivyo serikali inatoa pole kwa familia ambazo zimeondokewa na ndugu zao.
Aidha Naibu Waziri huyo amewaonya watu ambao wamekuwa wakitumia mitandao vibaya kwa kurusha taarifa za uongo ambazo zimekuwa zikipelea taharuki kubwa kuhusu maafa kwani taarifa hizo zinajenga hofu kwa wananchi.
"Inapotokea taarifa za maafa wapo wasemaji wake kwa mkoa ni Mkuu wa mkoa na wilaya ni Mkuu wa wilaya sasa wapo watu wanarekodi na kusambaza taarifa za uongo kwenye mitandao na kusababisha taharuki kubwa niwaombe achaneni na hii tabia tumieni mitandao vizuri" Alisema Naibu Waziri Ummy.
Naibu Waziri huyo, pia ameiagiza Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Moshi kukaa pamoja na kamati ya maafa ya wilaya pamoja na wataalam wengine kuzibua njia za mto Nanga na mto Manguvu ili kuzuia mafuriko katika kijiji cha Samanga kata ya Old Moshi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Moshi vijijini, Prof. Patrick Ndakidemi alitumia nafasi hiyo kuishikuru serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hasani kwa jinsi ambavyo wamezikimbilia familia za waathirika wa mafuriko.
Prof. Ndakidemi alisema kuwa, katika maafa hayo yaliyosababishwa na mvua jumla ya watu watano walifariki dunia pamoja na mashamba na vitu mbalimbali vikiwemo vyakula kusombwa na mafuriko.
"Msaada uliotolewa na serikali utasaidia kuzifariji familia ambazo zimekubwa na mafuriko pamoja na kuwafariji watu ambao ni wahanga kutambua jinsi ambavyo serikali inawathamini" Alisema Prof. Ndakidemi.
Naye Kaimu Mkuu wa wilaya ya Moshi, Amir Mkalipa aliwataka Watumishi wa halmashauri kuhakikisha wanagawa vitu hivyo kulingana na maelekezo ya serikali na yeyote atakayekiuka hatosita kumchukulia hatua.
Kwa upande wao waathirika waliishukuru serikali kwa jinsi ambavyo wamewakimbilia katika kipindi chote cha maafa hayo.
Msaada uliokabidhiwa na Naibu Waziri Ummy Nderiananga ni pamoja na mahindi tani 20, magodoro 150, mablangeti 150, ndoo 150, madumu 150, na mikeka 150.
Mwisho.
0 Comments