Header Ads Widget

RC SERUKAMBA ATAKA WANANCHI KUTOA USHIRIKIANO TAFITI ZINAZOFANYIKA SINGIDA

Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA

MKUU wa Mkoa wa Singida,Peter Serukamba,amezitaka kaya zilizochaguliwa mkoani hapa  kushiriki tafiti za kilimo, kiuchumi,kijamii na kutathimini upatikanaji endelevu wa huduma za maji, elimu ya afya na usafi wa mazingira kutoa ushirikiano makarani na wadadisi ambao wameanza kazi hiyo katika halmashauri zote za mkoani hapa.


Akizungumza na waandishi wa habari leo (Disemba 13, 2023) amesema serikali kupitia ofisi ya Taifa ya Takwimu imeanza tafiti hizo katika mikoa yote nchini ukiwamo wa Singida ili kuiwezesha nchi kupata takwiku rasmi ambazo zinatumika katika kutunga na kuhuisha sera,kupanga mipango,programu za maendeleo,kufuatilia na kutathimini utekelezaji wake.


Serukamba amesema katika utafiti es kilimo wa mwaka 2022/2023,utafuatilia maendeleo ya sekta ya kilimo nchini kwa kukusanya taarifa kuhusu hali ya kitaifa ya uzalishaji mazao,idadi ya mifugo na mazao yatokanayo na mifugo,utoaji wa huduma na matumizi ya rasilimali ilu kuongoza utekelezaji wa sera na mipango ya serikali kuhusu sekta ya kilimo.


"Utafiti huu wa kilimo ni muhimu sana kwa kuwa sekta ya kilimo inachangia wastani wa asilimia 26.2 ya pato la taifa,inatoa ajira karibu asilimia 65 ya watu wote nchini,inatuhakikishia usalama wa chakula na ina mchango mkubwa kwa maendeleo ya sekta nyingine hususani sekta ya viwanda," alisema.


Kuhusu utafiti wa kutathimini upatikanaji wa huduma za maji,elimu ya afya na usafi wa mazingira 2023, alisema utaisaidia serikali na wadau wa maendeleo kuelewa changamoto zinazokabili upatikanaji wa huduma hizo na kuchukua hatua stahiki za kuziimarisha,kuongeza upatikanaji wake na kuinua viwango vya ubora.

Serukamba alisema utafiti wa shughuli za kiuchumi na kijamii wa mwaka 2023, unafanyika ili kupata idadi ya shughuli za kiuchumi na kijamii zilizopo katika sekta iliyo rasmi na kupata muhimili wa sampuli ambao utatumika kama muongozo wa watafiti mbalimbali.


"Tafiti hizi zinatumika kufanya uchambuzi wa kina wa kiuchumi kama kupima tija kwenye uzalishaji,kutathimini mwenendo wa uchumi na zitasaidia katika uundaji wa sera kwa kutumia taarifa sahihi na maamuzi sahihi," alisema.


Serukamba alisema chini ya sheria ya takwimu,wajibu wa mwananchi ni kutoa ushirikiano kwa wadadisi wa tafiti hizi kwa kutoa majibu sahihi ya maswali yatakayoulizwa kwani hii si mara ya kwanza kwa wananchi wa Mkoa wa Singida kushiriki tafiti za kitakwimu.


Naye Meneja Takwimu,Ofisi ya Taifa ya Takwimu  Mkoa wa Singida,Naing'oya Kipuyo, alisema tafiti hizi kwa mkoa huu zimeanza tangu Novemba mwaka huu ambapo makarani na wadadisi wamesambazwa katika halmashauri zote saba za mkoa wa Singida.


Kipuyo alisema katika utafiti wa kilimo mwaka 2023, kaya 300 za kilimo zitahojiwa katika maeneo 25 na kwamba zoezi hilo litachukua miezi miwili.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI