Baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi ya kata ya Gwarama wilaya ya Kakonko wakiwa kwenye maandamano ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MKOA Kigoma unaelezwa kupiga hatua kubwa katika kudhibiti vitendo vya ukatili kwa makundi mbalimbali huku mkakati ukiwekwa kuhakikisha vitendo hivyo vinatokomezwa kabisa.
Mkuu wa mkoa Kigoma,Thobias Andengenye amesema hayo katika kilele cha maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili ambazo kimkoa zimefanyika kwenye Kijiji cha Gwarama wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma.
Katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Mkuu wa wilaya Kakonko, Kanali Evance Malasa alisema kuwa utafiti wa idadi ya watu na makazi wa mwaka 2015/2016 unaonyesha kuwa mkoa Kigoma ulikuwa na asilimia 42 ya vitendo vya ukatili ambavyo takwimu za mwaka 2022/2023 zinaonyesha kuwa vimeshuka na kufikia asilimia 34.
Kutokana na takwimu hizo alisema kuwa serikali ya mkoa kwa kushirikiana na wadau na wananchi itaendelea kutekeleza mipango ya kupunguza ukatili kwa kutekeleza afua mbalimbali ikiwemo kutoa elimu,kuchukua hatua za kisheria lakini pia kushirikisha makundi mbalimbali kwenye utekelezaji wa kupinga vitendo hivyo.
Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi Sekretariet ya mkoa Kigoma anayeshughulikia afya,Dk. Jesca Leba alisema kuwa Pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kupinga vitendo vya ukatili mkoani Kigoma kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo MTAKUWA mipango Zaidi imewekwa kuhakikisha mikakati iliyowekwa inatekelezwa na kufanikiwa.
Akizungumza katika maadhimidho hayo Afisa ulinzi na usalama kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF) ofisi ya Kigoma,Enna Lutengano alisema kuwa mafanikio ya mkoa Kigoma katika kudhibiti vitendo vya ukatili kunatokana na kutekelezwa kwa mifumo na mipango ambayo serikali, wadau wa maendeleo na wananchi wanatekeleza kwa Pamoja.
0 Comments