Header Ads Widget

MTAFUNGWA AWATAKA WAGANGA WA KIENYEJI KUSHIRIKIANA NA JESHI LA POLISI

NA CHAUSIKU SAID,MATUKIO DAIMAAPP MWANZA.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbrod Mtafungwa amewataka waganga wa kienyeji kushirikiana na jeshi hilo kuwasaidia kutokomeza mauaji yatokanayo na imani za kishirikina, migogoro ya ardhi, mauaji ya kujichukulia sheria mkononi, pamoja na unyang'anyi wa kutumia silaha.


Ameyabainisha hayo wakati akizungumza na waganga wa tiba asilia zaidi ya 500 katika ukumbi wa Gandhool na kueleza kuwa waganga hao wahakikishe wanatoa elimu Kwa jamii inayowazunguka ili kuhakikisha wanapunguza matukio ya mauaji na uhalifu.

Mtafungwa ameeleza kuwa waganga hao wanapaswa kuachana na ramli chonganishi Kwa kuwa ndio chanzo kikubwa Cha mauaji yenye sura za imani za kishirikina na kuona utaratibu huo umepitwa na wakati.


"Tunatamani kuona uharifu unaisha katika Mkoa wa Mwanza ili ifike hatua matukio ambayo yanakuwa yakileta hofu katika jamii yetu yanaisha mfano mauaji ya kutokana na imani potofu za kishirikina, migogoro ya ardhi, matukio ya ukatili wa kijinsia kwa watoto, kuwania mali, unyanganyi, wizi, pamoja na utapeli na ndio maana tumewaita leo ili kuzungumza na kuona namna gani mnaweza kusaidia katika kupunguza vitendo hivyo kwa sababu nyie ni kundi muhimu," amesema kamanda Mutafungwa. 

Mkuu  wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Mwanza, Mrakibu mwandamizi wa Polisi Yesaya Sudi amewataka waganga wa tiba asilia kuwafichua waganga bandia na wapiga ramli chonganishi katika jamii kwani wao ndio wamekuwa chanzo cha kuchafua sifa ya taaluma hiyo. 


"Niombe kwenye eneo hilo ukibaini mtu ambaye anapiga ramli chonganishi usimuache salama kwa sababu atakuwa anachafua kundi lenu pia mkiona mtu hana cheti wala taaluma ya tiba hiyo toa taarifa mapema ili asije kuwachafulia kundi lenu" amesisitiza mwandamizi Sudi 

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Waganga wa tiba asilia mkoa wa Mwanza, Shabani Ramadhani akizungumza kwa niaba ya kundi hilo ametoa wito kwa waganga wenzake kutoa taarifa ya waganga wale wasiofuata sheria huku akimpongeza Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu Hospitali za Rufaa kuwa na kitengo cha tiba asilia. 


"Niwaombe waganga wenzangu wa tiba asilia tusivunje sheria za nchi, tuendelee kujiendeleza kusoma katika vyuo vya waganga wa tiba asilia lakini kwa upande wa Serikali na Jeshi la Polisi kuzidi kutoa elimu hii na wasiishie mjini tu bali pia waende hata vijijini kwa sababu huko wengi wao hawajawai kufikiwa na elimu kama hii tunayopatiwa," amesema Ramadhani

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI