MWAKILISHI wa Jimbo la Mwanakwerekwe Ameir Abdallah Ameir, amesema, ni vyema wajamii kuendelea kuwaunga mkono watoto yatima na kuzitatua changamoto zao mbalimbali zinazowakabili ili kuendelea kupata kheri zaidi.
Akizungumza katika ugawaji wa sadaka ikiwemo Yunifom, viatu na mikoba ya skuli kwa watoto yatima wanaosimamiwa na jumuiya ya kuendeleza Uislamu na kusaidia Jamii Zanzibar (JUKUZA) hafla ambayo ilifanyika katika viwanja vya magogoni.
Alisema, watoto yatima wamekuwa na hali ngumu hivyo ni vyema wanajamii kuwa na mwamko wa kuendelea kuwalea watoto yatima ili kuona changamoto zinazowakabili ziweze kutatulika.
Aidha alihakikisha anaendelea kushirikiana na viongozi wa jumuiya hiyo ikiwemo kusaidia vijana katika ujasiriamali sambamba na kusoma kitabu kitukufu cha Allah.
"Jumuiya kama hizi zimekuwa zikisaidia sana wanajamii kwani wamekuwa wakiwahimiza watoto kusoma elimu zote mbili kwani viongozi mara nyingi wamekuwa wakipiga kelele za kuona vijana wanasoma elimu zote" alisema
Mapema, Mwenyekiti wa Bodi ya Jumuiya hiyo, Saidi Hamad Bakari, alisema ili uislamu uiendelee na ni vyema jamii kuendelea kuhimizana kukisomq kitabu kitakatifu cha Quran Tukufu sambamba na kuwaendeleza vijana katika masuala mbalimbali ikiwemo kusoma kwa bidii.
Alisema vijana wengi wamekuwa wakipuuza kusoma kitabu kitukufu ambapo vijana wengi hawaijui Quran, hivyo alisema watahakikisha wanajumuisha wanajamii katika kuwahimiza watoto kwenda madrasa.
Sambamba na hayo, alisema lengo la jumuiya ni kuisaidia jamii na kuwapatia elimu ya wajasiriamali na kuwasisitiza kuendelea kushirikiana kwa pamoja ili lengo liweze kufikiwa.
Akisoma risala katibu wa jumuiya hiyo, Asaa Mohamed, Asaa, alisema ugawaji wa vifaa hivyo ni moja ya nia na malengo yao ya jumuiya na kusema kitendo hicho ni kutasaidia kuwashajihisha watu wengine kuona wanaendelea kuwasaidia watoto yatima.
Aidha alisema jumuiya yao imekuwa ikitekeleza masuala mbalimbali ikiwemo kushughulikia watoto yatima, wajane na watu wasiojiweza.
Mbali na hayo, alisema changamoto zinawakabili ikiwemo muitiko mdogo katika harakani zao, ufinyu wa eneo wanalofanyia shughuli zao na wamekosa mtaji wa kufanyia shughuli zao jambo ambalo linasababisha kuomba wakati wa kufanya shughuli zao, hivyo, aliwaomba wahisani mbalimbali ili kutatua changamoto zao zinazojitokeza.
Katika hafla hiyo mwakilishi Ameir amechangia shilingi milioni moja kwa ajili ya kuendeleza masuala mbalimbali katika jumuiya na kuahidi kuwajengea jengo lao la kudumu sambamba na kuwapatia printa na komputa kwa ajili ya kuendeleza ufanisi wa kazi zao za kila siku.
0 Comments