Na Fadhili Abdallah,Matukio Daima Media,Kigoma
KUFUATIA kifo cha mfanyabiashara wa Katoro mkoani Geita Mwenyeji wa wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma Enos Elias kuuawa katika mazingira ya kutatanisha akiwa mikononi mwa polisi na maafisa wa uhamiaji Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe amemtaka mkuu wa jeshi la polisi nchini kuunda tume ya makamishna wa jeshi hilo kuchunguza kifo hicho.
Zitto ametoa kauli hiyo akihutumia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa mwenge Kakonko Mjini mkoani Kigoma ukiwa mkutano wake wa kwanza katika ziara ya siku nane ya mkoani Kigoma ambapo amepinga kamati iliyoundwa na Mkuu wa mkoa Kigoma kuchunguza tukio hilo.
Katika mkutano huo Zitto alisema kuwa tume ya Kamishna itakayoundwa na Mkuu wa jeshi la polisi nchini ndiyo itatoa majibu ya uhakika ya jambo hilo sambamba na kuchukua hatua kutokana na mamlaka na madaraka iliyonayo kwenye jambo hilo.
Alisema kuwa hakubaliani na kamati iliyoundwa na Mkuu wa mkoa Kigoma kwa kile anachoamini kwamba haitatenda haki na badala yake itaficha mambo mengi kuwalinda wahalifu waliofantya tukio hilo.
Kiongozi huyo wa chama cha ACT Wazalendo alisema kuwa wakati tume ikifanya kazi yake ametaka kusimamishwa kazi kwa Mkuu wa polisi wilaya ya Kibondo sambamba na kuondolewa kwa maafisa uhamiaji wa wilaya hiyo ambao ndiyo chanzo cha mgogoro huo uliopelekea mauaji ya kijana huyo.
Pamoja na hao Zitto ametaka pia kuwajibishwa kwa Mkuu wa wilaya Kakonko ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo kwa kushindwa kuchukua hatua za haraka na madhubuti kuwashughulikia wakosaji wakati kila kitu kinajieleza wazi kuhusu ushiriki wa polisi na maafisa uhamiaji katika kifo cha mfanyabiashara huyo.
Awali Naibu Waziri kivuli Viwanda na biashara wa ACT, Julius Masabo ameitaka serikali kukomesha mauaji na manyanyaso yanayofanywa na maafisa uhamiaji mkoani Kigoma kwa wananchi wa mkoa huo kwa kigezo cha utata wa uraia wao.
Masabo alisema kuwa zipo sheria na taratibu za kuwahudumia raia wan je lakini maafisa hao wa uhamiaji na polisi wameona kigezo cha watu wengi kuwa na utata wa uraia ndiyo chanzo chao cha mapato kwa kuomba rushwa kwa watu wanaowakamata badala ya kufuata taratibu za kisheria.
0 Comments