Header Ads Widget

WILAYA YA KONGWA YAJIDHATITI KUTANGAZA UTALII





Na Hamida Ramadhani, Matukio Daima APP Dodoma


OFISI ya Mkuu wa Wilaya ya Kongwa kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo nchini imeandaa mbio za Marathon kwa lengo la kuutangaza mchango wa Wilaya hiyo na Tanzania kwa ujumla katika ukombozi wa nchi za Afrika. 


Kupitia mbio hizo Ofisi hiyo itaendelea kutoa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa kuyatambua maeneo ya kihistoria, kuyalinda, na kuyaendeleza ili kuenzi historia ya taifa na kuyafanya sehemu ya utalii wa kihistoria katika maeneo ya urithi wa ukombozi yaliyopo nchini.


Hayo yameelezwa leo November 15, 2023 jijini Dodoma na Mkuu wa Wilaya hiyo Remidius Mwema wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mikakati ya kuitangaza wilaya hiyo kupitia mbio za marathon zitakazoanza November 25, 2023 wilaya ya Kongwa mkoani hapa. 


Amesema mbio hizo za marathon ambazo zimepewa jina la "Kongwa liberation Marathon" imezingatia taratibu zote za marathon na kwamba zimegawanywa kwenye makundi ya Km 5, Km 10 na Kilometa 21 huku mgeni rasmi wa mbio hizo akitarajiwa kuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Damas Ndumbaro. 


Amesema Wilaya ya Kongwa imegusa ukombozi na historia ya harakati za ukombozi wa nchi za  kusini mwa Afrika zikiwemo Afrika ya Kusini, Zimbabwe, Angola na Msumbiji na hivyo kuwa na nafasi ya kujitangaza kama sehemu ya vivutio vya utalii. 


"Serikali itashirikiana na nchi tulizozipa hifadhi wakati wa harakati za ukombozi kwa kukarabati majengo yaliyotumika na wapigania uhuru wa Afrika ikiwa ni sehemu ya kuenzi mchango wao na kuitunza historia hiyo kwa ajili ya kizazi cha sasa na cha baadae” amesema 


Amesema kupitia Marathon Wilaya hiyo itatangaza fursa za Uwekezaji zilizopo ikiwemo  Kilimo, Viwanda, Ranchi ya taifa, Soko la kimataifa la mahindi Kibaigwa na Hoteli za kitalii . 


"Kwa kuwa Kongwa ni lango la kuingia makao makuu ya nchi tunategemea kuwa sehemu ya kivutio cha utalii na uhifadhi wa historia, hivyo tumetenga eneo la Pandambili kwa ajili ya Uwekezaji wa Viwanda, tunawakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza, " Amesema na kuongeza;


"Niwaombe wana Dodona na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki kikamilifu kuendelea kutangaza fursa zetu kama ambavyo Serikali yetu imekuwa ikijitolea  fedha kukarabati baadhi ya maeneo muhimu ya kihistoria kupitia wizara ya utamaduni, Sanaa na Michezo, "amesema.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI