UWT CHINI YA MWENYEKITI MAMA CHATANDA KUKATA RUFAA KUMSAIDIA MARIA
DED IGUNGA NA WENZAKE KIZIMBANI KESI YA UHUJUMU UCHUMI
Na Fadhili Abdallah,Matukio Daima App,Kigoma.
ALIYE kuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Athumani Msabila ambaye amehamishiwa halmashauri ya wilaya Igunga na Wenzake 10 wamefikishwa Mahakamani Kwa kesi ya uhujumu Uchumi .
Watuhumiwa hao ni pamoja na watumishi saba wa manispaa ya Kigoma Ujiji na maafisa wawili wa wizara ya Tawala za mikoa na serikali za mitaa Leo wamefikishwa Mahakama ya hakimu mkazi Kigoma na kusomewa mashitaka 11 ikiwemo shitaka la uhujumu uchumi na utakatishaji fedha kiasi cha shilingi milioni 463.5.
Mbele ya hakimu Mkazi Kigoma, Hassan Momba mwendesha mashitaka Wakili wa serikali, Anonisye Erasto aliieleza mahakama hiyo kwamba washitakiwa hao walitenda makosa hayo kwa kipindi cha tarehe 1 Juni 2022 hadi tarehe 5 Juni 2023.
Pamoja na hayo washitakiwa hao ambao hawakutakiwa kujibu chochote pia walisomewa mashitaka ya kula njama kwa nia ya kutenda kosa, kugushi nyaraka, kutakatisha fedha, kuisababishia serikali hasara ya shilingi milioni 463.5 na matumizi mabaya ya madaraka.
Waliopandishwa kizimbani na kusomewama mashitaka ambao walikuwepo mahakamani hapo ni Pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi wa manispaa ya Kigoma Ujiji, Athumani Msabila ambaye amehamishiwa halmashauri ya wilaya Igunga akiwa mshitakiwa wa kwanza.
Wengine ni washitakiwa saba watumishi wa halmashauri ya manispaa ya Kigoma Ujiji ambao ni Pamoja na Afisa mipango wa halmashauri hiyo,Ferdinand Filimbi, Mweka Hazina wa manispaa hiyo, Salum Saidi, Kombe Salum Kabichi , Frank Nguvumali, Jema Mbilinyi, Moses Zahuye, Joel shirima na mtumishi kutoka ofisi ya Mkuu wa mkoa Kigoma, Bayaga Ntamasambilo.
Aidha washitakiwa wawili watumishi wa Wizara ya Tawala za mikoa na serikali za mitaa waliofikishwa mahakamani hapo ni Pamoja na Aidan Mponzi na Tumsifu ambao walisafirishwa kutoka Dodoma kuletwa Kigoma kwa ajili ya kusomewa mashitaka yao wakielezwa ndiyo waliohusika kupelekwa kwa fedha hizo Kigoma Ujiji kuwa ni Aidan Zabron na Tumsifu Kachira.
Kesi hiyo namba 3 ya mwaka 2023 imeahirishwa hadi tarehe 20 mwezi huu kwa ajili ya kutajwa sambamba nali kutoa uamuzi mdogo kwa washitakiwa watano kama wanaweza kupata dhamana ambapo washitakiwa wote walirudishwa rumande.
0 Comments