Kwa mara nyingine tena mpenzi msomaji wa Matukio Daima App hii napenda tuendelee kujifunza masuala mbalimbali ya malezi, makuzi na tabia kama ilivyo ada. Katika makala haya tupate maelezo ya swali ambalo kila mmoja wetu hujiuliza: “akili ya mtoto inarithiwa kutoka kwa mama peke yake?”
Awali ya yote naomba kunukuu maelezo ya makala fulani ambayo imetembea sana katika makundi ya Whatsapp ili iwe sehemu ya mjadala huu:
“Children Inherit their Intelligence from their Mother not Father”
A mother’s genetics determine how clever her children are, according to researchers, and the father makes no difference. Women are more likely to transmit intelligence genes to their children because they are carried on the X chromosomes and women have two of these while men have only one. But in addition to this, scientists now believe genes for advanced cognitive functions which are inherited from their father may be automatically deactivated. A category of genes known as “conditioned genes” are thought to work only if they come from the mother in some cases and the father in other cases. Intelligence is believed to be among the conditioned genes that have to come from the mother.
Kabla sijaanza kudadavua niweke tafsiri bayana ya kichwa hicho cha makala, “Watoto hurithi akili kutoka kwa mama zao na sio baba zao”. Baada ya tafsiri hiyo, vema tukaangalia mambo ya msingi ambayo ni akili na namna inavyorithiwa ili tupate mawazo jumuishi kuwa watoto hurithi akili kutoka kwa mama zao na sio baba zao.
AKILI
Akili ni hali ya utambuzi wa kufanya jambo. Utambuzi unaomfanya mtu ang’amue/afikiri na kufanya kitu ndio hutupatia tafsiri nyepesi ya akili. Wapo wanaodhani kuwa ukifanya vema kwenye mtihani ndio una akili. Kimsingi, akili ni dhana inayoambatana na mambo mengi katika maisha mathalani uwezo wa kuimba, kutumia vema mwili (mf. Katika kuruka, kucheza, kukimbia,n.k), utatuzi wa mambo, uneni, utambuzi wa mahali, tathmini binafsi, kuhusiana na watu wengine, utambuzi wa mambo ya asili. Hata hivyo, yote hayo yapo kwa kila mmoja na hutegemea ingawa si yote yanafanyika kwa viwango vya juu.
Nitatumia kipimo kimojawapo cha akili kiitwacho [kwa Kiswahili kisicho rasmi] KIWANGO CHA AKILI ama Intelligence Quotient, kwa lugha ya kigeni. Kipimo hiki hutumiwa si tu na wanasaikolojia bali pia wanajamii wengine katika kutambua kiwango cha akili alichonacho mtu awe mtoto, kijana, mtu mzima au mzee. Kimsingi, kinachoangaliwa hapa ni utendaji kazi wa ubongo kwa kuzingatia umri wa akili na umri halisi wa mtu husika. Kwa mfano, ikiwa mtoto wa miaka 12 anafanya mambo yanayopaswa kufanywa na mtoto wa miaka 9, mtoto huyo ataonekana kuwa na UWEZO DUNI.
Ufafanuzi wake uko hivi ili kuelewa zaidi;
Umri wa akili una madarajia mbalimbali kama:
· Akili zilizopindukia (mtu mwenye kiwango cha akili, asilimia kati ya 144 na kuendelea).
· Uwezo wa juu sana (mtu mwenye kiwango cha akili, asilimia kati ya 130 na 144).
· Uwezo wa juu (mtu mwenye kiwango cha akili, asilimia kati ya 115 na 129).
· Uwezo wa wastani wa juu (mtu mwenye kiwango cha akili, asilimia kati ya 100 na 114).
· Wastani wa chini (mtu mwenye kiwango cha akili, asilimia kati ya 85 hadi 99).
· Uwezo duni (mtumwenye kiwango cha akili, asimilia kati ya 70 na 84).
· Taahira kiasi (mtu mwenye kiwango cha akili, asilimia kati ya 55 na 69).
· Mtindio wa ubongo (mtu mwenye kiwango cha akili, asilimia kati ya 0 na 55).
Sasa basi ili kupata mfano wa hesabu ndogo niliyoitolea jawabu UWEZO DUNI unafanya hivi;
Unachukua umri wa akili unaugawa na umri wa kuzaliwa kisha unazidisha kwa silimia mia moja; 9/12 × 100% = 75. Katika maelezo hapo juu utakuwa umeona ninachokisemea. Katika mazingira kama hayo, je mtoto akiwa na uwezo duni tujumuishe pia mamaye ndivyo alivyo? Jibu linaweza kuwa ndiyo au hapana kutegemeana na mtazamo ulionao mwenyewe.
Tunapoendelea kudadavua kuhusu urithi wa akili katika masuala ya ‘kijenetiki’, ikumbukwe kuwa kromozomu hufanya kazi ya kudhibiti asili ya mtu. Zaidi ya yote, sehemu ya asili/tabia ya mtu hurithiwa pindi yai la mwanamke linaporutubishwa baada ya kukutana na manii/mbegu za kiume. Sehemu ya asili/tabia kama upole, ucheshi, ukorofi, uwezo wa kuchambua vitu, ukarimu, na kadhalika hurithiwa wakati huo huo kutoka pande zote mbili.
Ni kweli kuwa mwanamke ana XX kromozomu, tofauti na alivyo mwanaume mwenye XY kromozomu. Tena ni wazi kuwa mtoto wa kiume anachukua XY kromozomu ilhali mtoto wa kike huchukua XX kromozomu. Sasa basi, kwa vile kromozomu zinahusika na masuala ya jinsi, akili na masuala mengine ya kitabia, si vema kuja na hitimisho kuwa ‘watoto hurithi akili kutoka kwa mama zao na si baba zao.’ Ni vema, mpenzi msomaji, ukatambua ya kuwa si wakati wote mama anayeonesha ukarimu kwa wageni anapopata mtoto lazima pia mtoto awe mkarimu kama mamaye. Vipi inawezekana kweli mama mwanahisabati mzuri lazima mwanae pia awe mwanahisabati mzuri? Je, ni kromozomu za mamaye ndizo zinazohamisha akili kwenda kwa mtoto?
Ninao mfano wa Ben Carson, daktari bingwa mstaafu katika masuala ya mishipa midogo ya fahamu (Neurosurgeon). Historia ya Ben inaonesha kuwa hapo awali hakuwa ‘vizuri’ sana kimasomo katika ufaulu. Wakati huo huo, mama yake Ben, Sonya Carson aliyesoma madarasa matatu tu alikuwa na uwezo mkubwa wa utambuzi wa mambo pamoja na hisabati hali iliyopelekea kumjengea mwanaye, Ben mazoea ya kujisomea vitabu mara mbili kwa wiki pamoja na kuimba ‘tables’. Hali iliyopelekea, baadaye, Ben kufanya vizuri sana katika masomo na utambuzi wa mambo ya asili pamoja pamoja na utatuzi wa mambo kupitia ‘operesheni’ kadhaa alizofanya kwa wagonjwa. Kwa mfano huu, umhusuo Ben kufanya mambo katika mazingira wezeshi je ni sehemu ya akili ya mama yake, Sonya Carson?
Pengine, kwa minajili tu ya uelewa wa masuala ya kitafiti, kutokana na nukuu ya awali kuna changamoto za wazi katika maelezo hayo. Mchango wangu kama mchambuzi ni huu kufuatia makala hiyo;
Mosi, makala imetumia kigezo cha u-jinsi zaidi katika kuonesha uhusiano uliopo baina ya akili za mtoto na urithi toka kwa mamaye. Kimsingi, mtoto hawezi kurithi tabia ikiwemo akili kutoka upande mmoja tu (rejelea maana ya akili). Kama mwanamke na mwanaume wamekutana kimwili na matokeo yake yakawa kutengeneza ‘kiumbe’, ni wazi kuwa kiumbe kitengenezwacho kitakuwa na tabia tofauti tofauti. Huenda ikiwa utafiti ulifanyika na matokeo yakawa hayo, mwanamke amepewa nafasi hiyo kutokana na sababu ya kuambatana (attachment) zaidi na mtoto muda mwingi katika suala la malezi.
Pili, katika tafiti ili upate mrejesho utumikao kutoa matokeo ya tafiti za kitakwimu (quantitative research) ni vema kuonesha idadi kubwa/sampuli ya watafitiwa iliyotumika pamoja na mbinu ya/za ukusanyaji data. Kauli iliyotumika katika nukuu niliyoianisha ni ‘kauli jumuishi’ yenye maneno yaliyo na ukakasi pasi na kuonesha namna data zilivyokusanywa pamoja na idadi/sampuli ya watafitiwa.
Tatu, hata kama matokeo ya utafiti uliofanywa yamekuwa kama nukuu ilivyo, bado katika tafiti si wakati wote matokeo yaliyopatikana sehemu A yafanane na sehemu B. Ndiyo kusema, mtafiti anapaswa kuangalia, pamoja na mambo mengine, suala la ufanano wa kimazingira anapotaka kuhamisha matokeo ya utafiti wa sehemu A kwenda sehemu B.
Makala haya yameandaliwa na:
Mhadhiri Msaidizi wa Saikolojia na Utafiti,
Chuo Kikuu cha SAUT – Archbishop James University College, Songea.
novertydeograthias@gmail.com
0 Comments