Na Fadhili Abdallah, Kigoma
Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe ameitaka serikali kutumia sera, sheria na taratibu za nchi katika kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji nchini ambayo imekuwa na athari kubwa kwa maisha ya watu na kwamba mjgogoro hiyo isipotatuliwa sasa kinyume chake inaweza kuleta athari ya vita nchini.
Kabwe alisema hayo akihutumia mkutano wa hadhara kwenye kijiji cha Rukoma wilaya ya Uvinza mkoanj Kigoma Mwambao wa kusini wa ziwa Tanganyika na kusema kuwa migogoro hiyo inatatulika lakini viongozi wa serikali hawajatimiza wajibu wao katika kutekeleza utatuzi wa migogoro hiyo.
Alisema kuwa ipo sheria ya ardhi namba nne na namba tano ya mwaka 1999, ipo mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji na ipo mipango mikakati (master plan) ya maeneo mbalimbali anashangazwa kuona migogoro ikizidi kuongezeka badala ya kwisha.
Aidha kiongozi huyo ameshutumu viongozi wa vijiji kuwa chanzo cha migogoro ya ardhi na migogoro kati ya wakulima na wafugaji kwa kutoa maeneo bila kufuata sheria hivyo amewataka wananchi kutowachagua viongozi wa vijiji ambao wamekuwa tatizo kubwa la maendeleo yao. Sambamba na hilo Kabwe ameitaka serikali na Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC) kuyagawa majimbo ya Kasulu Vijijini na Kigoma Kusini mkoani Kigoma ili kusogeza uwakilishi na huduma kwa wananchi kutokana na ukubwa majimbo hayo.
Akiwa jimbo la Kasulu Vijiji Zitto alihutubia mkutano wa hadhara katika kijiji cha Kagera Nkanda ambapo alilazimika kutembea kilometa zaidi ya 200 kwenda kijiji cha Kalela ndani ya jimbo hilo kufanya mkutano wa hadhara aidha alifanya Mkutano mwingine wa hadhara katika mji wa Uvinza ambapo mkutano mwingine ndani ya jimbo hilo kijiji cha Rukoma alilazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilometa 300.
Awali Waziri kivuli wa ardhi wa ACT Wazalendo, Petro Ndolezi alimweleza kiongozi huyo wa chama kuwa kumekuwa na migogoro mikubwa ya kugombea maeneo baina ya wakulima na wafugaji ambapo wakulima wamekuwa wakinyanyasika kutokana na uwezo wa kifedha wa wafugaji kwa kutoa rushwa kwa viongozi wa serikali na polisi wanaosimamia masuala ya ulinzi na usalama.
Mwisho.
0 Comments