Na Matukio Daima App
BAADA ya Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kutengua uteuzi kwa aliyekuwa naibu waziri wa katiba na sheria Paulina Gekul ,mashirika yasiyo kuwa ya kiserikali mkoani Iringa yamempongeza Rais Samia kwa uamuzi wake mzuri huku yakitaka chama cha mapinduzi (CCM) kuchukua hatua za kuunga mkono hatua hiyo kwa kumvua ubunge na uanachama Gekul .
Raphael Mtitu katibu mtendaji asasi ya ICISO Iringa
Wakizungumza na Matukio Daima Media katibu wa shirika lisilo la kiserikali la ICISO mkoani Iringa Raphael Mtitu na katibu mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali la Caringi Hearts (CAHE) Jameda Kulanga walisema kuwa hatua iliyochukuliwa na Rais Dkt Samia imechukuliwa kwa wakati mzuri na imezingatia utawala bora na wao kama asasi za kiraia wanaungana na Rais katika hatua hiyo nzuri iliyochukuliwa .
Mtitu alisema kuwa baada ya kupata taarifa ya naibu waziri huyo kufanya vitendo vya uzalilishaji walipokea kwa mtazamo touati sana hasa kuona mtuhumiwa ni kiongozi mwenye jukumu kubwa kwa Taifa katika kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia nchini .
Hivyo alisema kuwa wao kama wanaharakati wa masuala la kupambana na ukatili wa kijinsia nchini walikuwa wakisubiri kuona hatua nzuri za kiuwajibishaji kama hizo zikitolewa japo kabla ya Rais kufikia uamuzi wa kutengua uteuzi wake walitarajia naibu waziri huyo angejiwajibisha kwa kujiuzulu nafasi zake zote kupisha uchunguzi .
Alisema kuwa chimbuko la unyanyasaji huo zinatajwa kuwa ni ugomvi wa kibiashara kati yake na mpiga kura wake jambo ambalo ni kinyume na kazi na wajibu wa mbunge na wapo wabunge wengine na viongozi wengi wenye maslahi kama hayo majimboni ya kugeuza majimbo yao kama sehemu ya biashara na hivyo kupelekea migongano ya kimaslahi kati yao na wapiga kura wao .
" Huyo mbunge ama diwani ni mwakilishi wa wananchi bungeni ama kwenye vikao vya baraza la madiwani sasa kama mwakilishi wa wananchi anafanya shughuli zinazofanana na wananchi kwenye eneo alilochaguliwa ni chanzo cha vurugu kama hizi jambo ambalo si sawa lazima achague moja kati ya siasa ama biashara mbunge lazima awe na heshima ya wapiga kura wake "
Mtitu alisema kuwa ndio maana kwenye katiba mpya wananchi wengi wanapigania kuona mbunge hawi mali ya chama bali anakuwa mali ya wananchi ili kuweza kumuwajibisha pale anapokosea .
Alisema kilichofanywa na mbunge huyo ni taswira ya wazi kuwa kuna haja ya kuwa na katiba mpya itakayomuwezesha mpiga kura kumwajibisha mbunge wake moja kwa moja .
Hata hivyo alisema kuwa mbali ya kuwa naibu waziri huyo anatokana na chama cha siasa ni vyema chama anachokiwakilisha kumchukulia hatua kali ikiwemo ya kumchukuliwa hatua za kumsimamisha ama kumvua uanachama wakati huu wa uchunguzi wa tuhuma dhidi yake .
" Gekul amechafua sana sifa ya chama tawala kwa kutanguliza mambo binafsi na kuacha misingi ya chama hicho ambacho kinajinasibu kutetea haki za binadamu wote sasa kama Rais amechukizwa na kuchukua hatua tunasubiri uamuzi wa chama chake kinachomdhamini nacho kuchukua hatua kama kweli kinaunga mkono uamuzi uliochukuliwa na Rais Dkt Samia " alisema
Mtitu alisema kuwa iwapo chama chake kinachomdhamini ubunge wake lazima kuchukua hatua za haraka kama ambavyo Rais alivyochukua hatua za haraka dhidi ya naibu waziri huo kama sehemu ya fundisho kwa wabunge na viongozi wengine .
Katika hatua nyingine Mtitu alisema kuwa viongozi kama Gekul ndio wamekuwa kikwazo kikubwa katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia nchini Tanzania kwani pale ambapo wanaharakati wa kupinga ukatili wa kijinsia wakipambana kutokomeza ukatili wao wamekuwa chimbuko la kuficha uovu ama kutetea kwa kuwa na wao ni wahusika wakuu wa ukatili kama huo ndio maana leo Mungu ameamua kumfichua Gekul ndani ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia .
Kwa upande wake katibu mtendaji wa shirika la CAHE Jameda Kulanga alisema kuwa viongozi kama hao wanarudisha nyuma mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia nchini kwani walitegemea kuona viongozi wanakuwa mfano wa kupinga na kukemea ukatili wa kijinsia nchini .
Hata hivyo alisema hatua ya kutumbuliwa kwenye nafasi yake ya unaibu uwaziri ni nzuri na itawafundisha viongozi wengine kutotumia vibaya vyeo vyao japo bado anashangazwa kuona hadi leo Gekul ni mbunge kimsingi baada ya kutenguliwa nafasi hiyo kubwa alipaswa kujiuzulu mwenyewe kabla ya kusubiri kutumbuliwa hata ndani ya chama .
Wakati huo huo wanaharakati wa kutetea haki za binadamu (Groundera) chini ya kiongozi wao Deusdedith Soka wametoa tamko kwa vyombo vya habari la kulaani vitendo vya kikatili alivyofanyiwa kijana Hashimu Ally Philimon Novemba 11 mwaka huu jimboni Babati mjini .
Wanaharakati hao wamesema wanalaani unyama huo na kuomba vyombo vya usalama kufanya kazi yake ya kuchukua hatua dhidi ya wahusika wa tukio hilo ili iwe fundisho kwa wengine .
0 Comments