Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA
BENKI ya NMB imezindua kampeni ya Teleza Kidijitali-Weka na Ushinde ambayo inalenga kuwahamasisha wateja wa benki hiyo kujenga utamaduni wa kuweka fedha na akiba kwenye akaunti zao kwa ajili ya manufaa yao ya sasa na ya baadaye.
Meneja wa NMB Kanda ya Kati, Janeth Shango akizungumza juzi wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya kampeni hiyo uliofanyika mjini Singida, alisema benki hiyo imekuja na kampeni hiyo baada ya kutambua kuwa uwekaji wa akiba kwa watanzania imekuwa jambo gumu hali inayosababisha panapotokea jambo linalohitaji fedha wanalazimika kutafuta mikopo ya haraka ambayo inakuwa na riba kubwa.
"Suala la uwekaji wa akiba linazidi kuwa kubwa na sisi kama benki ya NMB inayowajali wateja wake tumeona tuje na kampeni hii ambayo kwa namna moja au nyingine inaweza kusaidia idadi kubwa ya wateja wetu kuwa na tabia ya kujiwekea akiba ili wasipate wakati mgumu wanapokumbana na masuala yenye udharura," alisema Shango.
Shango alisema kupitia kampeni hiyo Benki ya NMB inaendelea kuhamasisha wateja wake kutotumia akaunti zao kama sehemu tu ya kufanya miamala na kupitisha pesa bali wazitumie vyema kujiwekea akiba na kuhifadhia pesa kwani kufanya hivyo watanufaika baadae.
" Ili kurudisha faida tunayoipata kama benki kwa wateja wetu tumezindua promosheni hii itakayoshuhudia zawadi ya pesa taslimu ambayo itawekwa katika akaunti zao ili kuwahamasisha kuendelea kuwa na akiba katika akaunti zao," alisema.
Kwa mujibu wa Shango alisema kampeni hiyo itakuwa na droo za kila wiki na utaratibu wa zawadi utakuwa ni kuongeza kiasi kilichopo kwenye akaunti yako kwa mara mbili kwa mshindi.
"Ni kwamba kama mteja atakuwa na Sh.Milioni moja kwenye akaunti yake na ameibuka mshindi, basi sisi NMB tutamuongezea shilingi milioni moja nyingine, tofauti na kampeni iliyopita kampeni hii tumeamua kuwa na zawadi ya aina hii ili kuhamasisha zaidi kutumia akaunti za NMB kwa ajili ya uwekaji wa akiba.
Aliongeza kuwa kampeni hii ambayo imeanza kutekelezwa Novemba 8, 2023 itaendelea mpaka wiki ya pili ya mwezi Disemba na ni mahsusi kwa wateja wote wa NMB kwa akaunti za akiba na zile za matumizi ambazo ndio za kawaida na hata kwa wale watakaojiunga na benki hiyo katika kipindi cha kampeni hii.
"Sisi kama NMB tutaendelea kuhamasisha matumizi ya akaunti za NMB kama njia ya kuhifadhi fedha na kujiwekea akiba ili kupata nafasi ya kushinda zawadi hizo na hivyo kufanya kipindi cha kuelekea mwisho wa mwaka kuwa chenye manufaa zaidi," alisema Shango.
Alisema Benki ya NMB inazohuduma bora za kidigitali ambazo zinamanufaa kwa mteja ambazo ni huduma ya Mshiko Faster ambayo mteja anaweza kujipatia mkopo mpaka Sh.500,000 papo hapo bila kufika kwenye tawi la benki kuweka dhamana yoyote.
Alitaja huduma nyingine inayotolewa na benki hiyo ni ya 'Spend to Save' ambayo inamuwezesha mteja kuweka akiba kwa kila tumizi lake kwenye akaunti yake na huduma ya NMB Pesa Akaunti ambayo mteja anaweza kufungua akaunti mpaka kwa Sh.1000 na tayari anakuwa na vigezo vya kujipatia huduma zingine zinazotolewa na benki hiyo.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt.Fatma Mganga akizindua kampeni hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, aliishukuru Benki ya NMB kwa kuja na kampeni hiyo ambayo itatoa elimu kwa wananchi wakipata fedha zao zitakuwa salama na kuzalisha zaidi kwa kuweka akiba na hivyo kuchangia maendeleo ya mkoa huo.
Úwekaje wa fedha kwenye akaunti za NMB ni jambo jema na linapaswa kupokelewa kwa mikono miwili na kama unafikiri kuweka akiba sio ujanja basi kutokuweka akiba ukipatwa na tatizo utaona mziki wake na ndio utajua umuhimu wa kuweka akiba," alisema Dkt.Mganga.
Alisema suala la uwekaji akiba ni la muhimu sana katika maisha yetu kwani mara nyingi yamekuwa yakiibuka mambo ya dharura yanayohitaji fedha na unapokuwa huna akiba utaona ugumu wa kutatua tatizo husika.
Katika uzinduzi huo Benki ya NMB ilitoa zawadi mbalimbali kwa washindi wenye akaunti kwenye benki hiyo ambapo mshindi namba moja Pascal Saba alizawadiwa jokofu kubwa na simu janja huku mshindi wa pilu akizawadiwa simu janja.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Mgoma Lake Ltd,Martin Mtinda alikabidhiwa trekta la mkopo kutoka benki hiyo lenye thamani ya Sh.Milioni 27.
Alisema gharama za trekta hiyo Benki ya NMB imemlipa asilimia 80 na mkulima atalipa asilimia 20 ambazo atalipa ndani ya miaka mitatu.
0 Comments