![]() |
Mheshimiwa Hussein Bashe, Waziri wa Kilimo |
Wananchi na wakazi wa eneo la Katesh
Wilaya ya Hanang mkoani Manyara wafurika katika barabara kuungojea Msafara wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassani ambapo
Rais alipata wasaa wa kusikiliza kero zao.
Katika msafara huo wakazi wa Katesh watoa
malalamiko yao juu ya upandaji wa bei za mbegu za kilimo kwa baadhi ya
makampuni wakati maeneo mbalimbali nchini wakielekea katika msimu wa kilimo
ambapo katika kulijibia hilo Rais Samia amsimamisha waziri wa Kilimo Mheshimiwa
Hussein Mohamed Bashe kutoa ufafanuzi juu ya changamoto ya bei za mbegu za
kilimo.
Kwa mujibu wa Waziri mwenye dhamana ya
kilimo Mheshimiwa Bashe ametoa ufafanuzi wa jambo hili kwamba ameshawapa kazi
maalum Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) kuhakikisha
ifikapo Oktoba 20 mwaka huu wawe wameshatoa bei elekezi ya mbegu hususani mbegu
za mahindi kwa nchi nzima na kwa kila eneo.
Mheshimiwa Bashe amesikitishwa na kitendo
cha baadhi ya makampuni yanayojihusisha na uzalishaji wa mbegu za kilimo, kuuza
mbegu zao kwa gharama za juu kwani serikali inatoa maeneo, miundombinu na
baadhi ya huduma za muhimu kuhakikisha makampuni haya yanazalisha mbegu kwaajili
ya kuwasaidia wakulima na sio kuwakandamiza kwa namna moja ama nyingine.
Aidha Waziri wa kilimo Mheshimiwa Bashe
ameahidi kuyafutia leseni makampuni ya mbegu yatakayokwenda kinyume na
maelekezo na maagizo kuhusu bei elekezi ya bei za jumla na bei ya rejareja
baada ya kutangazwa siku hiyo ya tarehe 20 oktoba, pia ameyaasa makampuni ya
mbegu kuhakiksha yanatoa kwenye magazeti bei elekezi kama walivyokubaliana.
Hata hivyo katika kuhakikisha utekelezaji
wa suala hili Waziri Bashe amesema Serikali kupitia Wizara ya kilimo itatoa
vibali kwa wakuu wa wilaya kutembelea maduka ya uuzaji wa mbegu kuhakiki
utekelezaji wa agizo hilo na kuchukua hatua za kuyafunga maduka yote
yatakayokwenda kinyume na agizo hilo.
0 Comments