Na Derick Milton, Bunda-Mara.
Kutokana na uwepo wa Changamoto ya Mabadiliko ya tabia nchi, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imewasisitiza wakulima wa zao la mpunga nchini kutumia teknologia ya kilimo shadidi kwenye zao hilo ili kukabiliana na Mabadiliko hayo pamoja na kuzalisha kwa tija.
Sekta ya kilimo nchini ni Moja ya eneo ambalo limeadhiriwa na Changamoto hiyo, kutokana na kupungua kwa mvua, ongezeko la ukame, kuongezeka kwa wadudu washambuliao mazao pamoja na udongo kukosa rutuba ya kutosha.
Akizungumza na wakulima pamoja na Maafisa ugani Katika Skimu ya Umwagiliaji ya Maliwanda Wilayani Bunda Mkoani Mara Mtafiti Uchumi na Jinsia kutoka TARI Dkt.Theodore Kessy amesema ili wakulima wa zao la mpunga nchini waweze kukabiliana na Changamoto hiyo wanashauliwa kutumia teknologia ya kilimo Shadidi.
Dkt. Kessy ameongeza kuwa Kilimo shadidi kwenye zao la mpunga ni teknologia ambayo upandikizwa miche michanga yenye umri kuanzia siku 8 hadi 14, hupandwa mche mmoja kwenye shimo, kwa nafasi pana sentimeta 25 kwa 25 na mkulima utakiwa kufanya palizi kwa kutumia vipalizi umwagiliaji wa kulowesha na kukausha shamba, pamoja na kuweka mbolea.
Amesema kuwa teknologia hiyo ni Muhimu kwani Mkulima analazimika kulima eneo dogo lakini ana uwezo wa kuvuna mazao mengi ikiwa atafuata kanuni zote zinazotakiwa “ Kwenye hekari Moja mkulima anaweza vuna wastani wa mpaka Tani 10 hi ni sawa na tani 4 kwenye ekari moja ya mpunga”
Naye Mtafiti na Mgunduzi kutoka TARI Dkt. Juliana Mwakasendo amebainisha kuwa teknologia ya Kilimo Shadidi ni tofauti sana na kilimo cha kawaida, kwani hakihitaji maji mengi, ambapo ameeleza Mkulima atatakiwa kuweka maji kwenye shamba lake pale tu itakapohitajika kuwekwa maji.
" Tunajua kwenye kilimo cha kawaida cha zao hili wakulima ugombania hadi maji maana kila mmoja uhitaji maji mengi, lakini Kilimo shadidi Mkulima uhitaji maji kidogo, maji yanawekwa kwenye shamba pindi tu yanapokauka ndipo mkulima anatakiwa kuweka mengine, siyo kila wakati shamba limejaa maji,” ameeleza Dkt.Mwakasendo.
Amewashauri wakulima wa zao hilo nchini kubadilika na kuona kama ni zao la kibiashara kwa kuacha kulima kwa mazoea, huku akisisitiza matumizi ya teknologia hiyo itasaidia kuzalisha kwa tija, uwepo wa uhakika wa chakula, kukua kwa pato la taifa na kuongeza ajira hasa Kwa vijana na akina mama.
TARI inatekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wakulima na maafisa Ugani juu ya teknologia ya kilimo shadidi kwenye zao la mpunga kupitia vituo vyake vya Uyole, Ifakara na Mikocheni katika Wilaya za Mbarali, Iringa vijijini, Bunda vijijini, Kilombero na Pwani.
Mradi huo unaofadhiliwa na Norwegian Agency for Development Cooperation unalenga kuwajengea uwezo wa Kitaasisi juu ya mifumo ya uzalishaji wa zao la mpunga inayokuabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, pamoja na rasilimali kwa ufanisi kwa kuzingatia kilimo shadidi.
0 Comments