Na fatma Ally, Matukio DaimaApp, Dar
Katika kuhakikisha Serikali inalifufua shirika la ndege la Tanzania (ATCL) leo inapokea ndege mpya aina ya Boeing 737 MAX 9 yenye uwezo wa kupokea abiria 181na kubeba mizigo tan 6 ambapo inafikisha ndege 13 zinazomilikiwa na Serikali tangu lilipoanza kufufuliwa shirika hilo 2016, ambapo Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango kesho Oktoba 3, anatarajia kuwaongoza Watanzania kupokea ndege hiyo.
Aidha, Dk. Mpango anatarajia kukabidhi ndege mbili za injini moja aina ya Cessna Skyhawk 172 kwa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), lengo likiwa ni kuendeleza Kituo cha Umahiri katika Uendeshaji wa Usafiri wa Anga na Usafirishaji.
Akizungumza jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kuhusu ujio wa ndege hiyo na zile za mafunzo amesema mwaka 2021 Serikali iliiwezesha NIT kuingia mkataba wa ununuzi wa ndege mbili ndogo za mafunzo ya urubani aina ya Cessna Skyhawk 172 zinazotumia injini moja.
Aidha, kuhusu ndege mpya ya ATCL amesema itachukua abiria 181, ambapo ndege hiyo ina madaraja mawili, la abiria 165 na daraja la abiria 16, ujio huo wa ndege hiyo ATCL itafikisha ndege 14 mpya.
Amesema kuwa, ujio huo wa ndege itawezesha vituo vya Pemba, Tanga, Mbeya, Nachingwea na Musoma, ambapo itatengeneza mruko wa ndege saa za usiku, huku leo Oktoba 2, wakitarajia kuanzisha safari za usiku mkoani Dodoma.
Amesema ndege hizo zilitengenezwa na Kampuni yaTextron Aviation ya Marekani, ziliwasili nchini Januari mwaka huu zikiwa zimevunjwa, kwa sasa zimekamilika kuundwa na zipo tayari kuzinduliwa na tayari kwa kuanza kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa urubani.
"Zilikuja katika vipande vidogo vidogo zikaunganishwa hapa kisha ndiyo unapata hizi ndege. Kila moja inaweza kubeba watu wanne ikijumlisha rubani zitatumia mfumo wa kisasa ambao unamuwezesha rubani kuratibu taarifa kiurahisi na hivyo kuongeza umakini na usalama wakati wa urushaji wa ndege,"amesema Prof. Mbarawa.
Aidha, amesema chuo hicho kitatumia ndege hizo kutoa mafunzo ya urubani kwa daraja la awali ambayo yatachukua miezi sita na ya leseni ya CPL yatachukua miezi 12 kwa gharama ndogo ikilinganishwa na gharama za mafunzo hayo nje ya nchi.
Ameongeza kuwa, kwa wastani kwa mwanafunzi mmoja kwa kozi zote mbili takribani Sh milioni 300 zilikuwa zikitumika, lakini kwa kuja ndege ndogo hizo bei itashuka sana kwa kuwa ndege moja inaweza kufundisha wanafunzi watano, chuo kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 10 kwa wakati mmoja.
Naye, Naibu Mkurugenzi wa Huduma za Uchukuzi, Biseko Chiganga amesema Serikali imewapa NIT eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa ajili ya kujenga hanger ambayo itatumika kwa masomo ya urubani wakiwemo marubani.
“NIT itajenga shule ya urubani KIA na kwa wakati huo chuo kitakuwa kinatumia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa mafunzo ya vitendo,” amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amewataka wananchi kujitokeze kuipokea ndege hiyo ikiwa ni ishara ya kumuunga mkono Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kutokana na kazi anayofanya.
0 Comments