Header Ads Widget

ASILIMIA 90 YA WATANZANIA WANAKULA CHAKULA CHA SUMU - MNYETI

Alexander Mnyeti - Naibu Waziri Mifugo na Uvuvi


 

Na Fadhili Abdallah, Kigoma

 

NAIBU Waziri wa mifugo na uvuvi Alexander Mnyeti amesema kuwa idadi kubwa ya watanzania wanakula chakula cha nafaka chenye sumu kuvu  hivyo kuitaka Wakala wa Taifa wa hifadhi ya chakula (NFRA) kufanya utafiti wa teknolojia rahisi itakayowezesha utunzaji wa mazao ya nafaka kwa wananchi vijijini yanayozingatia usalama wa chakula.

 

Mnyeti amesema hayo Mjini Kigoma alipotembelea banda la NFRA kwenye viwanja vya Mwanga Community Centre Mjini wakati akizindua maadhimisho   ya siku ya chakula duniani ambayo kitaifa yanafanyika mkoani Kigoma Oktoba 16 mwaka huu Mnyeti ameitaka NFRA kutafuta teknolojia rahisi vijijini itakayowezesha uhifadhi wa mazao ya nafaka unaozingatia usalama wa chakula.

 

Mnyeti alisema kuwa NFRA imekuwa na uhifadhi mzuri wa chakula kwa mazao ya nafaka lakini uhifadhi huo zaidi unafanyika kwenye maghala yanayosimamiwa na wakala huo lakini kwa wananchi wa kawaida wamekuwa wakihifadhi na kutumia nafaka mbalimbali bila kuzifanyia taratibu za kuondoa sumu zilizomo kwenye nafaka hizo.

 

Kutokana na hali hiyo Naibu Waziri huyo ameitaka NFRA sambamba na kutafuta teknolojia rahisi ya kuhifadhi chakula inayozingatia usalama wa chakula lakini pia ametaka watendaji wa wakala huo kwenda vijijini kutoa elimu kwa wakulima na wananchi jinsi ya kuvuna,kuhifadhi na  kutumia chakula kinachotokana na nafaka  bila kuwepo kwa sumu kwenye chakula hicho.

 

Mikalu Mapunda - Mkurugenzi wa masoko NFRA.


Akitoa maelezo kwa  Naibu Waziri alipotembelea banda lao

Mkurugenzi wa masoko wa NFRA,Mikalu Mapunda amesema kuwa kwa sasa wakala huo una teknolojia ya kisasa ya kuhifadhi nafaka ambayo haiweki sumu kuvu na kufanya mazao na nafaka zinazohifadhiwa na wakala huo kuwa salama kwa chakula kinachotengenezwa.

 

Hata hivyo amekiri kuwepo kwa changamoto kubwa kwa wananchi vijijini katika kujua kiwango cha sumu kuvu kilichopo kwenye mazao yao kwani  sehemu kubwa ya nchi vijijini hakuna vipimo vya kupima sumu kuvu na ili kujua uwepo wa sumu kuvu kwenye mazao alisema kuwa  kazi hiyo imekasimiwa kwa Shirika la viwango  nchini  (TBS) ambao wamekuwa wakikagua na kuangalia ubora wa mazao na uhifadhi wake kulingana na viwango vilivyowekwa na kwamba watazingatia ushauri wa Naibu Waziri kutafuta taknolijia rahisi ya kujua uwepo wa sumu kuvu kwenye mazao.

 

 

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS