Na WILLIUM PAUL, MOSHI.
Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi ameshiriki adhimisho la Siku ya Wazee Duniani kwa mwaka wa 2023 iliyofanyika katika viwanja vya Radio Kicheko Live katika Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani mwaka huu wa 2023 ni “Uthabiti wa Wazee Kwenye Dunia yenye Mabadiliko”.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Radio Kicheko Live Dr Heavenlight Kavishe aliwakaribisha katika hilo tamasha la Tabasamu ya Wazee.
Katika hafla hiyo, wazee walishiriki shughuli mbalimbali ikiwemo kula vyakula vya asili vya Kichaga, kufanya mazoezi ya kutembea, kucheza nyimbo za asili ya kichaga, kucheza twisti, kuvuta kamba, kukimbia na maji kichwani na kukimbia na yai lililowekwa kwenye kijiko kilichokuwa kimewekwa mdomoni.
Akiwasalimu wazee, Mbunge Ndakidemi amewaahidi wazee kuwa ikimpendeza Mwenyezi Mungu, atakuwa anashiriki nao kila mwaka na kuwaomba wazee kushiriki kikamilifu kwenye kulisaidia taifa kujenga na kulinda maadili ya vijana wetu.
Katika mazungumzo yao, wazee wamemuomba Mbunge aiombe Serikali itunge sheria na sera ya wazee ili iweze kuwasaidia.
Pia wameiomba serikali kuwapatia Pensheni Jamii wazee wote wenye umri mkubwa ili waweze kujikimu katika mahitaji yao ya kila siku.
Wazee wameitaka serikali kuwapatia wazee vitambulisho vya matibabu bila malipo kwani wanakabiliwa na magonjwa mengi yanayohatarisha maisha yao na wengi wao hawana uwezo wa kujitibu.
Akijibu hoja zao, Mbunge aliwaambia kwamba serikali iko katika mchakato wa kutunga sheria ya wazee na kuboresha sera ya wazee ya mwaka 2003 na kuwahakikishia kuwa atafikisha changamoto zote walizompa kwenye mamlaka husika.
Wazee walipata fursa ya kupima afya zao kwani kulikuwa na kibanda cha madaktari kutoka hospitali ya Rufaa ya KCMC ambao waliwahudumia wazee.
Mada mbalimbali zilitolewa na wataalamu ambazo zilihusu lishe bora kwa wazee na magonjwa hatarishi kwa wazee. Mada nyingine zilihusu uwekaji wa akiba ambazo zilitokewa na ELCT ND SACCOS na Benki ya Uchumi.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na Madaktari bingwa na wataalamu wa lishe kutoka Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Viongozi wa ELCT SACCOS, Mkuu wa mkoa mstaafu Kanali Enos Mfuru, Wazee kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kilimanjaro na Mikoa jirani ya Manyara na Arusha.
Mwisho..
0 Comments