NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
MTAKWIMU Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita imewekeza katika sekta ya Afya hali inayopelekea Mtanzania anayezaliwa sasa umri wake wa kuishi hapa Duniani kuwa ni miaka 65 huku Mwananchi wa mkoa wa Kilimanjaro umri wake wa kuishi ukiwa ni miaka 63.
Dkt. Albina ametoa kauli hiyo leo wakati wa Semina ya Usambazaji na uhamasishaji wa matumizi ya matokeo ya Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwa Viongozi, Watendaji na Wadau wa mkoa wa Kilimanjaro iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha Polisi Moshi (CCP).
Alisema kuwa, kwa mujibu wa sensa ya mwaka 1978 ilionyesha umri wa kuishi kwa Mtanzania ni miaka 44 ambapo hii yote imechangiwa na kiasi kikundwa na uwekezaji unaofanyika na Serikali ya awamu ya sita katika sekta ya Afya.
Mtakwimu huyo alisema kuwa, pato la Taifa linaendelea kukua kwa asilimia 5.2 ambapo kwa mkoa wa Kilimanjaro wastani wa pato la mtu kwa mwaka ni milioni 4 kwa mwaka huku kwa wastani wa kitaifa ni milioni 2.8.
"Tuipongeze Serikali ya awamu ya sita kwa jinsi inavyojikita katika kuinua sekta mbalimbali lengo likiwa ni kuhakikisha watanzania wananufaika na rasilimali zao" alisema Dkt. Albina.
Aidha Mtakwimu huyo alisema kuwa, katika sekta ya Elimu tunaendelea kufanya vizuri na hii inatokana na juhudi kubwa za Rais Dkt. Samia Suluhu Hasani ambapo kiwango cha kujua kusoma na kuandika kimeongezeka ambapo asilimia 80 ya Watanzania wanajua kusoma na kuandika na kwa mkoa wa Kilimanjaro asilimia 94 wanajua kusoma na kuandika.
Dkt. Albina alisema kuwa, yote hayo yamechangiwa na uwekezaji mkubwa uliofanywa katika sekta ya Elimu hali inayopelekea wananchi kutembea kifua mbele kwani Elimu ndio kila kitu na kudai kuwa hadi kufikia sensa ya mwaka 2032 watanzania wote watakuwa wanajua kusoma na kuandika.
Kwa upande wake, Kamisaa wa Sensa Tanzania Bara na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda amesisitiza matumizi sahihi ya takwimu zilizotokana na zoezi la Sensa ya watu na makazi.
Anne alisema kuwa, Watanzia asilimia 99.99 wamehesabiwa na kutumia nafasi hiyo kuwapongeza Watanzania ambapo sensa ya sasa ilikuwa ya kisasa ambapo Rais Dkt Samia Suluhu Hasani aliagiza kutengenezwa kwa mwongozo wa matokeo ya Sensa.
"Serikali ilituagiza kutengeneza mwongozo wa namna ya kutekeleza matokeo ya Sensa kwa watu wenyewe ambapo tunafundisha wananchi wajue kile walichokifanya kinamaana gani katika maisha yao kama mtu mmoja mmoja kama taasisi kama kitongoji inamaana gani" alisema Anne.
Alisema kuwa, kwa mujibu wa takwimu asilimia 57 ya wanakilimanjaro wananguvu ya kufanya kazi sawa na watu milioni 1.7 na kuwataka Watanzania wengine kufikia Kilimanjaro na kuacha tabia ya utegemezi.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Takwimu Zanzibar, Balozi Amina Salum alisema kuwa, Sensa ni kitu endelevu na ni nyenzo muhimu ya kupanga maendeleo ya Nchi.
Balozi Amina alisema kuwa, semina hiyo inalengo ya kufundana jinsi ya kutumia matokeo yaliyotokea kwenye sensa.
"Sensa ni kitu endelevu na ni nyenzo muhimu ya kupanga maendeleo yetu ya nchi na ndio maana kwa mwaka 2022 uongozi mzima wa Taifa ulijikita katika zoezi la Sensa na Leo tunajifunza jinsi ya kusoma hizi takwimu na kuzijua ili kuzitumia kama nyenzo za maendeleo yetu" alisema Balozi Amina.
Mwisho..
0 Comments