Fatma Ally, Matukio DaimaApp, Dar
Watanzania wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika kilele cha kumbukizi ya kifo cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yatakayofanyika katika hifadhi ya Msitu wa Kazimzumbwi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mratibu wa maadhimisho ya kumbukizi wa Julius Nyerere ambae pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Uhifadhi wa Mazingira (CODECO) Steven Nchimbi, amesema wameamua kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kuandaa Matembezi katika Hifadhi ya Kazimzumbwi wilayani Kisarawe ikiwa ni sehemu ya kumbukizi ya miaka 24 tangu kifo cha aliyekuwa baba wa Taifa Hayati Julius Nyerere.
Amesema kuwa, lengo la matembezi hayo ni kutangaza utalii uliopo katika hifadhi hiyo pamoja na kuviangalia vivutio vyake, hivyo amewataka wananchi mbalimbali kujitokeza katika matembezi hayo ili kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muunguano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika kukuza sekta ya utalii nchini Tanzania.
Hata hivyo, amewataka wadau wa mazalia ya misitu kufika katika hifadhi hiyo ili kuweza kuangalia vivutio mbalimbali vilivyopo na kuweza kujifunza namna bora ya uhifadhi wa misitu sambamba na kufanya utalii wa ndani.
Kwa upande wake, Afisa wa TFS Catherine Melchiory amesema kwa kila mshiriki wa Matembezi hayo atapaswa kulipa gharama ya shilingi 35,000.
“Gharama ni 35,00 ikijumuisha chakula, usafiri, Burudani yani Live Band, ngoma za asili na Ma Dj wa Burudani,” amesema Catherine.
Catherine amebainisha kwamba mgeni Rasmi wa Matembezi hayo anatarajiwa kwa Waziri wa Maliasili na Utalii Angella Kairuki.
Aidha, amewataka wadau watakaotaka kushiriki kukata tiketi zao mapema ambapo amesema zinapatikana Mpingo House, Mwenge Vinyago chumba namba 15.
Amesema magari ya kwenda hifadhini yatapatikana Mlimani City, Mbezi Magufuli, Mpingo House na Oilcom Ubungo.
0 Comments