NA THABIT MADAI,ZANZIBAR
SIKU chache tangu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutangaza fursa za Uwekezaji wa Mafuta na Gesi Asilia katika eneo la Mangapwani lenye ukubwa wa Hekta 47.53, Kampuni ya Oryx Gas limited imeungana na Kampuni ya TP limited Zanzibar lengo likiwa kuimarisha Uchumi, Ugavi pamoja na Usambazaji wa Gesi Visiwani Humo.
Hatua hiyo inakwenda sambamba na adhma ya Rais Dkt Hussein Ali Mwinyi ya kuifungua Zanzibar kiuchumi pamoja na kuwawezesha Wananchi visiwni humo kutumia Gesi Asilia katika Matumizi yao ya Nyumbani.
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika hafla fupi ya kuunganisha Kampuni hizo ambayo imefanyika katika Hotel ya Park Hayyat Mjini Unguja, Mwenyekiti wa Kampuni ya Vigor ambae pia Mbunge wa Jimbo la Mpendao Tuafiq Salim Turkey amesema kuwa uwamuzi wao wa kuunganisha kampuni hizo utasaidia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa Uhakika wa Gesi Visiwani humo.
"Kampuni ya Oryx Limited imeungana na kampuni ya Tp Limited ya Zanzibar ambayo ni kampuni Tanzu ya Vigor Turky's Group ili kuimarisha Ugavi na usambazaji wa Gesi katika Visiwa hivi," amesema.
Ameeleza kwamba, hatua hiyo itasaidia kuboresha Afya na Ustawi wa Wananchi wa Zanzibar kutokana na kuimarisha njia mbadala na salama ambayo inakwenda kuondosha Matumizi ya Mkaa na kuni.
Ameongeza kuwa Sababu nyingine ya kuungana ni kufuatia uundwaji wa kituo cha Kwanza cha Gesi LPG Visiwani humo ikiwa na dhamira ya upatikanaji wa uhakika wa Gesi katika Soko la Afrika husuani Tanzania bara na Visiwani.
Aidha Amefafanua kuwa, Katika Makubalino ambayo wameafikiana ni pamoja na kujenga kituo cha Gesi chenye Uwezo wa MT 1,300 ambacho kitakamilika robo ya Nne ya mwaka 2023.
"Dhamira yetu ni kuhakikisha tunakuwa Mstari wa mbele katika kutoa bidhaa na huduma zenye hadhi ya kimataifa huku gharama nafuu ambayo jamii yetu inweza kuimudu," ameongeza.
Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx Gesi Tanzania Benoit Arama amesema kuwa, kutokana na Maubalino waliofikia Kampuni ya Oryx itanunua kwa asilimia mia mali za Biashara za Kampuni ya TP limited ambazo zinatambulishwa na kuendeshwa kwa jina la VGesi.
"Kampuni ya Oryx Gesi itanunua mali za biashara ya LPG za Kampuni ya TP limited ambazo kwa sasa zinatambulikana na kuendeshwa kwa jina la VGesi ambapo sasa mali hizi zitatambulishwa kuwa chini ya jina la Oryx Energies." ameeleza.
Amefafanua kuwa, Katika Makubaliani ya mkataba Kampuni ya TP limited itachukua asilimia 30 ya hisa za Oryx Gesi Zanzibar limited.
"Kwa muda mrefu tumekuwa tukiweka misingi mbalimbali ambapo kwa ushirikiano huu ni hatua ya muhimu ya kuimarisha zaidi Usambazaji wa Gesi Zanzibar," amesema.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Oryx Gesi Zanzibar Shuwekha Khamis amesema nia na dhamira yao ni kuhakikisha wakazi wa Zanzibar wanapata Nishati ya Gesi safi na kwa uhakika licha ya kuwa na changamoto mbalimbali katika usafirishaji.
"Ushirikiano na Kampuni kubwa ya ndani ya Nchi yanahakikisha dhamira yetu ya kuwapatia Wananchi Nishati safi ambapo itachagiza ukuwaji wa Uchumi kupitia Utalii," ameeleza.
0 Comments