Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Wakati halmashauri ya wilaya ya Njombe ikikiri kushindwa kufikia asilimia 100 ya makusanyo yake ya ndani katika mwaka wa fedha uliopita,Halmashauri hiyo imebuni chanzo kipya cha mapato kitakachoongeza makusanyo hayo.
Sababu zilizotajwa kushuka kwa makusanyo hayo ni kutokana na kushushwa kwa ushuru wa mbao kutoka shilingi mia mbili mpaka mia moja kwa ubao jambo ambalo limeilazimu halmashauri kubuni chanzo kipya kupitia sekta ya usafirishaji.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Njombe,Mwanasheria George Makacha amesema wameamua kumpa mwekezaji wa usafirishaji ardhi katika eneo lililopo Njombe Mjini kwa kumpangisha kwa muda anayeilipa fedha halmashauri hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Njombe,Kissa Kasongwa wakati akizundua ofisi za kampuni ya mabasi ya ABC zilizopo katikati ya mji wa Njombe amepongeza jitihada za halmashauri hiyo kupata mwekezaji mpya anayesaidia halmashauri kuongeza makusanyo.
Wawekezaji na watoaji wa huduma za usafirishaji mkoani Njombe waliowekeza katika halmashauri hiyo akiwemo Severine Ngallo wamesema wapo tayari kushirikiana na serikali katika nyanja mbalimbali za kusogeza mbele maendeleo ya nchi.
Nao wakazi wa mji wa Njombe wamesema adha ya kupata huduma za usafiri wakati wa safari zitakwenda kupungua kutokana na mmoja wa wawekezaji kufungua ofisi ya usafirishaji katikati ya mji.
Hata hivyo Mkoa wa Njombe umewahimiza Watanzania na wageni kutoka mataifa ya nje kufika mkoani hupa kwa ajili ya kuchangamkia fursa za uwekezaji kwenye sekta mbalimbali hali ambayo itasaidia kukuza uchumi.
0 Comments