NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
Mbunge wa Jimbo la Moshi vijijini Profesa Patrick Ndakidemi ameendelea kufuatilia utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa kukagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Kiboroloni - Tela - Maideni inayojengwa kwa kiwango cha changarawe ambapo serikali imetoa shilingi milioni 175 za kukarabati barabara yenye urefu wa Km 8.6.
Katika ukaguzi huo, Mbunge huyo alitembelea Kata ya Old moshi Magharibi na kuzungumza na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi wa Kata na Matawi na wale wa Serikali za Vijiji na Vitongoji.
Mbunge aliwaambia viongozi hao kwamba, katika bajeti ya 2023/2024, alipambana na kupatiwa shilingi milioni 175 kukarabati barabara hiyo kupitia mfuko wa TOZO.
"Viongozi na wananchi mlioko hapa, Mbunge wenu nilipambana kule bungeni mpaka nikapewa fedha hizo". Alisema Ndakidemi.
Akiongea kwenye ziara hiyo kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa CCM Kata, Godson Mchau alimwomba Mbunge kuwa katika ukarabati wa barabara, uwekaji wa moram kwa umbali wa Km 3.5 uanzie kwenye Ofisi ya Kijiji Maringeni kuelekea juu mlimani.
Vilevile, alieleza hofu ya kutumika moram isiyo na viwango na uwepo wa mitaro ya kuchepusha maji kutoka barabarani.
Akijibu hoja hizo, mwakilishi wa TARURA Wilaya Eng. Mchanga alikubali kubeba kero zilizojitokeza kwenye ukaguzi huo na aliahidi kuzifanyia kazi kama walivyoombwa.
Wakihitimisha ziara ya Mbunge, Katibu wa CCM Kata, Fredrick Saria kwa niaba ya wenzake walimshukuru Mbunge kwa kufuatilia utekelezaji wa mradi wa barabara yao.
Alisema, kwa kipindi kirefu (karibia miaka nane) barabara hiyo ilikuwa haijafanyiwa ukarabati mkubwa na kumwomba kumfikishia salamu kwa Rais Samia kwa kuwapatia pesa za kuitengeneza barabara yao.
Mwisho..











0 Comments