Header Ads Widget

BILIONI 42 ZAMALIZA KERO YA MAJI KIGOMA UJIJI




Na Fadhili Abdallah,Kigoma

 

SHILINGI Bilioni 42 zilizotumika kwa ajili ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji katika manispaa ya Kigoma Ujiji zinaelezwa kumaliza tatizo na kero kubwa ya maji iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa manispaa hiyo na vitongoji vyake.

 

Hayo yamebainishwa na kutolewa ushuhuda na wananchi wa manispaa hiyo kwa nyakati tofauti walipokuwa wakiongea na waandishi wa habari waliokuwa wakitembelea kuona hatua za utekelezaji wa mradi huo ambao ulitumika kama turufu ya kupata kura kwa vyama mbalimbali vya siasa kwenye jimbo la Kigoma Mjini.



Mmoja wa wananchi wa manispaa hiyo Anastazia Elias Mkazi wa Kibirizi alisema kuwa changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji kwa sasa imekwisha kwani waliteseka kwa muda mrefu kutafuta maji ya bomba wakati ziwa liko karibu yao.




Naye Tiba Ramadhani Mkazi wa Nazareth Manispaa ya Kigoma Ujiji alisema kuwa baada ya kukamilika kwa mradi wa maji sasa hivi upatikanaji wa maji umekuwa mkubwa kwenye nyumba zao hadi vyooni na kwenye mabomba ya kuogea na kuishukuru serikali kwa kazi kubwa ambayo imefanyika.


Akieleza kuhusu utekelezaji wa mradi huo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya maji safi na maji taka Kigoma Ujiji, Poas Kilangi alisema kuwa kwa sasa mradi mkubwa uliokuwa unatekelezwa umekamilika na upatikanaji wa maji Kigoma Ujiji na vitongoji vyake umeimarika ukifikia asilimia 90.

 

Kilangi alisema kuwa mradi huo uliotekelezwa kwa thamani ya shilingi Bilioni 42 kwa mkono nafuu wa Jumuia  ya Ulaya (EU) kwa sasa una uwezo wa kuzalisha lita milioni 42 kwa siku na kwamba kwa sasa uzalishaji unafanyika kufikia lita milioni 24 kulingana na hali ya mahitaji ya sasa.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI