Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MAMLAKA ya usimamizi wa bandari nchini imesema kuwa bandari za ziwa Tanganyika katika mikoa ya Kigoma,Katavi na Rukwa imekuwa na mchango mkubwa katika utendaji wa bandari ya Dar es Salaam katika kusafirisha shehena na abiria kwenda ndani na nje ya nchi.
Kaimu Meneja wa bandari za ziwa Tanganyika.Nasha Ezra amesema hayo wakati wa uzinduzi wa wiki ya maadhimisho ya miaka 18 ya kuanzisha kwa Mamlaka hiyo ambapo uzinduzi huo umefanyika kwa kutoa msaada kwenye hospitali ya mkoa Kigoma Maweni.
Ezra alisema kuwa miaka 18 ya utendaji wa TPA bandari hizo zimefanyika kazi kubwa nab ado Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kuboresha utendaji wa bandari hizo kuhakikisha zinafikika wakati wote na kuwa chachu kubwa katika kuongeza mapato ya serikali na kuinua uchumi wa nchi.
Akizungumza maadhimisho hayo alisema kuwa TPA ziwa Tanganyika imekabidhi jumla ya magodoro 44 na shuka 150 vyenye thamani ya shilingi milioni 10 ikiwa n sehemu ya mipango ya mamlaka hiyo kusaidia shughuli za kijamii kwa wadau wao.
Kwa upande wake Afisa Habari wa TPA Makao Makuu,Revina Kato akizungumza kwa niba ya Mkurugenzi mkuu wa TPA alisema kuwa misaada iliyotolewa ni sehemu ya shughuli mbalimbali zinazopamba madhimisho ambayo yanafikia kilele chake Septemba 16.
Akizungumza baada ya kupokea misaada iliyotolewa na TPA Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa Kigoma,Dk.Lameck Mdengo alisema kuwa magodoro na mashuka yaliyotolewa yanapunguza changamoto ya mahitaji ya vifaa hivyo hospitalini hapo.
Dk.Mdengo alisema kuwa uwepo wa magodoro ya kutosha yanaondoa changamoto iliyokuwepo huko nyuma ya wagonjwa wawili kulala kitanda kimoja au wagonjwa kulala bila shuka na kwamba mashuka na magodoro hayo yanachangia utoaji uwepo wa huduma bora hospitalini hapo
0 Comments