NA MATUKIO DAIMAAPP, VATCAN
Hatimaye historia imeandikwa. Baba Mtakatifu Francis amempa Hadhi ya Ukardinali, Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Tabora, Protase Rugambwa katika viwanja vya Mtakatifu Petro nchini Vatican leo Septemba 30, 2023.
Leo Maaskofu wakuu 21 kutoka nchi mbalimbali Duniani, wamepewa hadhi ya Ukardinali na mmoja wa maaskofu hao ni Protase Rugambwa.
Kardinali Rugambwa anakuwa Mtanzania wa tatu kupata wadhifa huo mkubwa baada ya Askofu Laurean Rugambwa, Mwadhama Polycarp Pengo na sasa Kardinali Protase Rugambwa.
Kardinali Protase Rugambwa ni mzaliwa wa Karagwe, Jimbo la Kayanga, Kijiji cha Kasheshe, Parokia ya Nyaishozi,mkoani Kagera.
Rugambwa anatoka katika ukoo wa Abakaraza (Abarigi). Majina yake ya kifamilia ni Protase Abakaraza.
Jina la Rugambwa alipewa kama heshima kwa Askofu Laurean Rugambwa ambaye alifanya ziara Bukoba siku ambayo alizaliwa Protase katika miaka ya 1960.
Baba yake Protase alihama Karagwe akawa anafanyakazi Bukoba mjini. Mama yake alipopata mimba na baadaye kujifungua May 31 mwaka 1960 siku ambayo Kardinali Laurean Rugambwa alifanya ziara ya kitume Bukoba.
Baba yake Laurean alikuwa Mkatoliki jadidi (A die hard Catholic adherent) akasema kwa kuwa mtoto wake huyo amezaliwa siku ambayo Kardinali Rugambwa amekwenda kwao, basi ataitwa kwa jina lake (Rugambwa).
Alibatizwa na kuitwa Protase Rugambwa. Na kama ambavyo jina hubeba tabia za mtu, hatimaye naye amekuwa Kardinali kama mwenye jina lake.
Biblia inasema heri kuchagua jina jema kuliko mali nyingi (Mithali 22:1). Kwa hiyo wazazi wapeni watoto wenu majina mazuri kabla ya kuwapa urithi wa mali.
Katika kuonesha mtangamano wa Kanisa (Church compatibility), Kardinali Rugambwa amesindikizwa Vatican na viongozi mbalimbali wa Katoliki pamoja na madhehebu mengine.
Mmoja wapo ni Askofu wa Kanisa La Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dr.Benson Bagonza ambaye amekwenda Vatican kushuhudia tendo hili kubwa kwa Kanisa na dunia kwa ujumla.
Askofu Bagonza alipopewa nafasi ya kusema neno kuhusu Kardinali Rugambwa amesema "Ni mtu ambaye hekima imemzidi kimo na utu umemtangulia mbele.
"Ni mnyenyekevu lakini si mdhaifu. Mwenye nidhamu, lakini si muoga.
Makardinali kwa nafasi zao ndiyo washauri wakuu wa Papa.
Tumuombee Kardinali Rugambwa katika wajibu wake huu mpya wa kuwa Mshauri wa Papa.
Roma Locuta, Causa Finita. Roma ikisema, mjadala unafungwa"
Mwisho.
0 Comments