Header Ads Widget

ACT WAZALENDO: PENSHENI IWE KWA WAZEE WOTE NCHINI

 




NA ARODIA  PETER,MATUKIO DAIMA App, DAR

Mwenyekiti wa Ngome ya Wazee wa Chama cha ACT Wazalendo, Mzee Yasin Mohammed amesema Serikali inao wajibu wa kuwahudumia wazee kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ili waweze kuishi maisha ya furaha.


Amesema utatuzi wa changamoto hizo ni pamoja na Serikali kutenga ruzuku kwa kuwalipa pensheni wazee wote nchini kwani walikwishatoa jasho lao kwa ajili ya kulitumikia Taifa wakati wa ujana wao.


Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 30, 2023, Makao Makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam, Mzee Mohammed amesema pia kuwa wazee nchini wanahitaji kupata uwakilishi kwenye vyombo vya maamuzi likiwamo Bunge na Halmashauri ili kusimamia maslahi ya wazee kwani kwa sasa wazee hawatambuliwi na kila fursa inayopangwa na serikali inakwenda kwenye makundi ya wanawake, vijana na wenye ulemavu.


“Kwa mfano wazee Tanzania wanazo changamoto nyingi zinazohitaji kutatuliwa na Serikali kwa kuwalipa pensheni ya kila mwezi kama inavyofanyika Zanzibar ambapo kila mwezi wazee wana kifuta jasho na sasa pensheni yao imepanda i kutoka Sh 20,000 hadi 50,000. Hili ni jambo jema kabisa.


Aidha katika mkutano huo ambao ni maalum kuelekea Siku ya Wazee Duniani ambayo hufanyika Oktoba Mosi kila mwaka, Mzee Mohammed pia amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kutumia siku hiyo kwa kutoa misamaha kwa wafungwa ambao ni wazee ili nao wafurahie siku hiyo kwa kurudi uraiani.


Amesema ingawa Rais hutumia mamlaka yake   kusamehe wafungwa katika Siku kuu zingine zikiwamo za Muungano, Uhuru na nyinginezo, lakini kwa umuhimu wa siku hii, Ngome ya Wazee wa ACT Wazalendo inamuomba kuiangalia kwa jicho la kipekee kwa kuwaachia wazee wanaotumikia vifungo gerezani.


“Tunaposherehekea Siku ya Wazee duniani, tunaikumbusha jamii ilitambue hili kundi la wazee kwamba linahitaji kupata huduma maalum, kwa mfano kwenye vyombo vya usafiri vya umma kama pantoni, mabasi ya mwendokasi wazeewaruhusiwe  wasafiri bure, huduma za vyoo pia waruhusiwe kuvitumia bila malipo”amesisitiza.  

“Tunapozungumzia pensheni hatujumuishi wazee  waliokuwa watumishi wa serikali, tunataka wazee wote watengewe ruzuku, walipwe pensheni kwa sababu walishalitumikia Taifa lao kwa nguvu zote, hakuna sababu ya kuwabagua,. Jambo hili kama linawezekana Zanzibar kwa nini Bara isiwezekane wakati nchi ni moja? amehoji Mzee Mohammed.


Wazee wa Ngome ya ACT Wazalendo wanatarajia kuadhimisha Siku ya Wazee Duniani katika Jimbo la Mkuranga mkoani Pwani kesho Oktoba Mosi, 2023.


Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi, Tanzania ina jumla ya watu milioni 61,741, 120, kati yao wazee ni milioni tatu sawa na asilimia 5.7 ya watanzania wote.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI