Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Wafanyabiashara wa vitenge mkoani Kigoma wamesema kuwa punguzo la kodi ya ongezeko la thamani kwa ajili ya uingizaji wa vitenge nchini kutoka nje ya nchi kutawawezesha kufanya biashara zao vizuri na kuondokana na kufanya biashara hizo kwa njia zisizo halali (Njia za panya).
Wafanyabiashara hao wameeleza hayo katika semina ya siku moja iliyotolewa na Mamlaka ya Mapato (TRA) ikieleza mabadiliko ya sheria za kodi mbalimbali kwa wafanyabiashara, mawakala wa forodha na wasafirishaji wa shehena mkoani Kigoma.
Mmoja wa Wafanyabiashara hao, Zera Yusuph kutoka soko kuu la Mjini Kigoma alisema kuwa punguzo la kodi ya ongezeko la thamani kutoka kulipa asilimia 50 ya uingizaji vitenge hadi kufikia asilimia 35 linawapa nafasi nzuri ya kufanya biashara halali na kuondoa mzigo mkubwa wa kodi walizokuwa wakitozwa hivyo kutumia njia halali kuingiza vitenge nchini.
Naye Mfanyabiasharabkutoka soko la Masanga mjini Kigoma, Kolelo Mabruki ameishukuru serikali kwa kupunguza kodi hiyo ambayo ilikuwa kilio kikubwa kwa wafanyabiashara ya vitenge na ndiyo sababu ya kuwafanya kutumia njia za panya kuingiza vitenge nchini.
Awali akitoa maelezo kuhusu marekebisho hayo ya kodi Afisa mwandamizi wa idara ya forodha ya Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Allan Maduhu alisema kuwa serikali imesikia kilio cha wafanyabishara hao na kuamua kufanya utafiti ambao umepelekea kupunguzwa kwa kodi hiyo ya uingizaji vitenge nchini.
Naye Meneja wa TRA mkoa Kigoma,Deogratius Shuma alisema kuwa kupunguzwa kwa kodi ya thamani ya uingizaji wa vitenge kutoka nje ya nchi na vinavyoingizwa nchini kutawezesha wafanyabiashara hao kutumia njia halali kuingiza bidhaa lakini pia kuondokana na kukimbiza na maafisa wa mamlaka hiyo.
0 Comments