![]() |
Na Fatma Ally, Matukio DaimaApp, Dar
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewataka wananchi kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinazotolewa na mamlaka hiyo kwa saa 24, ili waweze kufuatilia mwenendo wa mvua za vuli na tahadhari zinazotolewa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC) Dkt Ladislaus Chang’a amesema kuwa utabiri uliotolewa ni wa kipindi cha msimu wa miezi mitatu, octona hadi Disemba hivyo viashairia vinavyochangia mwenendo wa mifumo ya mvua na mabadaliko ya muda mfupi utazingatiwa katika uchambuzi wa utabiri wa muda wa kati na mfupi.
Aidha, amesema kuwa mvua za juu ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi ikiwemo mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, kusini mwa mkoa wa Simiyu, kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, Dar es Salaam, Tanga, Pwani (ikiwemo visiwa vya Mafia), kaskazini mwa mkoa wa Morogoro na pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba katika msimu wa mvua za Vuli, 2023.
Ameongeza kuwa, maeneo ya mikoa ya Mara, kaskazini mwa mkoa wa Simiyu, Arusha, Manyara na Kilimanjaro yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani, hivyo ni vyema wadau wa sekta mbalimbali wanatakiwa kufuata ushauri na tahadhari unaotolewa na mamlaka hiyo katika kipindi chote cha mwelekeo wa mvua za vuli kuanzia octoba hadi Disemba.
Amefafanua kuwa kutokana na uwepo wa El-Nino, vipindi vifupi vya mvua vinatarajiwa kwa mwezi Septemba, 2023 katika baadhi ya maeneo nchini, hata hivyo, mvua za Vuli, 2023 zinatarajiwa kuanza rasmi mwezi Oktoba, 2023 katika maeneo mengi.
"Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2023 katika maeneo ya magharibi mwa Ziwa Victoria na kusambaa katika maeneo mengine mwezi Oktoba, 2023, kwa kawaida mvua za Vuli huisha mwezi Disemba, hata hivyo msimu huu mvua za nje ya msimu zinatarajiwa kuendelea mwezi Januari, 2024, ongezeko la mvua linatarajiwa mwezi Disemba, 2023”amesema Dkt. Chang’a.
Aodha, Dkt. Chang’a amesema, mamlaka ya hali ya hewa Tanzania itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa mirejesho ya mwelekeo wa mvua nchini kadri inavyohitajika. Aidha, wadau wanashauriwa kuwasiliana na Mamlaka ili kupata taarifa mahsusi za utabiri wa msimu ili kukidhi mahitaji maalum katika sekta zao.
Msimu wa Mvua za Vuli ni mahususi kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro), pwani ya kaskazini (kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba), ukanda wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara) pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.
0 Comments