Header Ads Widget

MBUNGE WA JIMBO LA MOSHI VIJIJINI PROF. PATRICK NDAKIDEMI AENDELEA NA ZIARA YA KATA KWA KATA AFIKA KIBOSHO MASHARIKI.

 


NA WILLIUM PAUL, MOSHI.


Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi ameendelea na ziara ya kutembelea Jimbo lake la Moshi Vijijini kwa kutembelea  Kata ya Kibosho Mashariki  kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kusikiliza kero za wanachi.


Mbunge  huyo aliambatana na viongozi mbalimbali wa chama kutoka wilaya ya Moshi vijijini wakiongozwa na Ramadhani Mahanyu, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi Kata na wataalamu kutoka Serikalini.  



Akiwa katika mkutano wa hadhara Mbunge aliwashukuru wananchi kwa jinsi wanavyoiunga mkono Serikali inayoongozwa na Dr Samia Suluhu Hassan. 


Aliwaahidi kuwa ataendelea kuwatumikia kwa nguvu zake zote na kusikiliza na kutatua kero zao ambapo alisema kuwa  hadi kufikia sasa, kiasi cha shilingi bilioni 4,580,775,694.00 zimeelekezwa Kata ya Kibosho Mashariki katika miradi ya maendeleo.



 "Nimshukuru Rais Samia Suhuhu Hassan kwa namna anavyoendelea kutoa fedha za Maendeleo katika Kata ya Kibosho Mashariki na niwaombe wananchi miradi inayoletwa na Serikali muendelee kuitunza na kuilinda ili iweze kudumu muda mrefu" alisema Prof. Ndakidemi.


Katika mkutano huo Mbunge aligawa miche ya kisasa ya migomba kwa wananchi kama alivyokuwa ameahidi wakati wa kampeni na kuwahimiza wananchi kuchukua miche bora ya kahawa kutoka kwa Afisa Kilimo wa Kata ambayo ilikuwa katika eneo la mkutano.



Miche zaidi ya elfu kumi na moja ya kawaha iligawanywa ambayo imetolewa na Serikali na Shirika la KPL.


Akijibu kero za wananchi, Ndakidemi ameahidi kuwa yeye na Diwani watatafuta suluhu za kero za wananchi ambazo ni pamoja na ile ya wananchi wachache wanaojihusisha na uuzaji wa gongo na bangi, upatikanaji wa maji safi na salama, ubovu wa barabara za ndani, kukosekana kwa mawasiliano ya simu kwenye eneo linalopakana na mlima Kilimanjaro, kukosekana umeme kwenye baadhi ya vitongoji, kukarabatiwa mifereji ya asili na ukosefu wa mitaji kwa vijana.



Akifunga mkutano, Diwani wa Kata ya Kibosho Mashariki, Christopher Ndakidemi alisema kuwa wamefarijika na ugeni wa Mbunge na viongozi alioambatana nao, kwani umejibu maswali mengi ya wananchi wa Kata ya Kibosho Mashariki


Kwenye ukaguzi wa miradi, Profesa Ndakidemi alifanya ukaguzi wa jengo la kutolea mafunzo katika chuo cha usimamizi wa Wanyamapori Mweka ambapo aliridhishwa na utekelezaji wa  Mradi huo ambao umefikia asilimia 67 ili kukamilika. 



Ujenzi huo unafanywa na Kampuni ya SUMA JKT ambapo Naibu Mkuu wa Chuo hicho Prof Alex Kisingo alisema kuwa ujenzi wa Chuo hicho unatekelezwa kwa fedha za  Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa gharama ya Shilingi za Kitanzania bilioni 3,799,982,716.49 ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi bilioni 2,189,101,051.28 zimetumika.


Katika ziara yake, Mbunge Ndakidemi alikagua miradi ya ujenzi  wa hosteli ya wavulana katika Shule ya Sekondari Sungu, na ujenzi wa choo katika Shule ya  Msingi Mweka. 


Akiongea baada ya ukaguzi wa ujenzi wa hosteli hiyo, Mbunge alitoa rai kwa wazazi kuwa na mipango endelevu ambayo itawawezesha kujenga hosteli za kutosha ili wanafunzi wanaosoma katika Sekondari ya Sungu waishi kwenye mazingira ya hosteli ili waweze kuwa na muda wa kutosha kujisomea na kuwafanya wafaulu vizuri. 


Akiwa katika Shule ya Msingi Mweka, Mbunge alitoa mchango wa shilingi laki tano ili kukamilisha kazi ya kuingiza maji katika vyoo ambavyo ujenzi haujakamilika.


Mwisho...

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI