NA Gift Mongi MATUKIO DAIMA APP MOSHI
Mbunge wa jimbo la Moshi vijijini Profesa Patrick Ndakidemi amehitimisha ziara ya kukagua miradi katika baadhi ya kata za jimbo lake.
Katika ziara yake aliyoifanya tarehe 9/8/2023, Prof Ndakidemi alifanya ziara katika Kata ya Uru Kusini ambapo alitembelea na kukagua miradi miwili ambayo ni ujenzi wa bweni la wasichana katika shule Shule ya Sekondari Mawela na Ujenzi wa Kkituo cha afya cha Uru Kusini.
Akiwa katika Kituo Cha Afya, Prof Ndakidemi alimshukuru Rais Dr. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa T.Shs milioni 790 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho ambacho kiko katika hatua za mwisho kukamilika na kitaanza kutoa huduma tarehe 14.8.2023.
'Kipekee nimshukiru rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutupa fedha hizi hakika ni mapenzi mema kwa wananchi wa Uru Kusini na hatuna budi kuunga mkono jitihada anazozifanya katika kutuletea maendeleo'anasema
Aidha amesema kuwa Kituo hicho cha afya ni muhimu kwani kitawasaidia wananchi wa Uru Kusini na kata nyingine za jirani ambao walitaabika kupata huduma za kitabibu kwa umbali mrefu.
Pia aliishukuru serikali kwa kutoa shilingi milioni 20 za kujenga hosteli ya wasichana katika shule ya Sekondari Mawela kwani itakuwa mkombozi kwa watoto wa kike waliokuwa wanakutembea umbali mrefu kupata elimu, na kukumbana na adha mbalimbali ikiwemo ya kupata uja uzito.
Katika ziara yake, mbunge aliongozana na Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini n Ramadhani Mahanyu, Mbunge wa viti maalumu mkoa wa Kilimanjaro Shally Raymond, Diwani wa Kata ya Uru Kusini Wilhad Kitaly, viongozi wa CCM Kata na Matawi ya Uru Kusini.
Akiongea na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kitandu, Prof Ndakidemi alieleza wananchi idadi ya miradi iliyotekelezwa kwenye Kata yao kwani hadi sasa zimetumika zaidi ya shilingi bilioni 1.7. Katika idadi hiyo, haikujumuisha miradi ya umeme, maji na elimu bure.
Miradi iliyotekelezwa iko kwenye sekta za elimu, Afya, ustawi wa jamii na miundombinu ya barabara.
Katika mkutano wake, Mbunge aligawa miche ya kisasa ya migomba na akawaomba wananchi wa Uru Kusini kujiandikisha au kuboresha taarifa zao katika mfumo wa kielektroniki kwa ajili ya kupata mbolea ya ruzuku kwa msimu ujao wa kilimo.
Wakieleza kero zao, wananchi walilalamika kuwa kero yao kubwa ni ubovu wa miundombinu ya barabara.
Kero nyingine kubwa ni uharibifu unaofanywa na wanyama waharibifu wa mazao kama Kima, Tumbili na Ngedere.
Kwa nyakati tofauti, Mheshimiwa Diwani na Mbunge walijibu kero zote zilizotolewa na wananchi. Waliahidi kuzifanyia kazi na kuzifikisha katika mamlaka husika.
Mbunge Ndakidemi alitoa mchango wa shilingi laki tano kusaidia ujenzi wa ofisi ya kijiji cha Shinga ambapo Shally Raymond alimuunga mkono kwa kuchangia shilingi laki moja.
Katika mkutano huo, Katibu wa CCM Wilaya ndugu Ramadhan Mahanyu aliwaomba wananchi waendelee kukiunga mkono Chama Cha Mapinduzi, Rais Samia Suluhu Hassan, Mbunge na Diwani kwani maendeleo waliyopata kwa kipindi kifupi yanaonekana.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi waliohudhuria katika mkutano huo, Diwani wa Kata ya Uru Kusini Wilhad Kitaly alimshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za maendeleo katika kata yao.
Vilevile, alimpongeza Mbunge wao Prof. Ndakidemi kwa jinsi ambavyo anawapigania wananchi na kuwaunga mkono katika kuwaletea maendeleo.
0 Comments