Header Ads Widget

BASATA YATAMBULISHA MABALOZI WAKE, ACCES KUFANYIKA DAR NOV 9 - 11

 



Na Fatma Ally, Matukio DaimaApp, Dar 


Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limewatambulisha rasmi mabalozi wake watakaoshirikiana nao katika kutangaza kazi zinazofanywa na baraza hilo ndani na nje ya Tanzania lengo ikiwa ni kuwafikia wadau wengi zaidi wa tasnia ya sanaa.


Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam wakati akiwatambulisha mabalozi hao, Katibu Mtendaji wa BASATA Dkt. Kedmon Mapana amesema kuwa, miongoni mwa malengo ya baraza hilo ni kupanua wigo wa mawazo na kutangaza Falsafa yake iliyojikita katika kufufua, kukuza na Kuendeleza zaidi Sekta ya Sanaa na kuipa mawanda mapana ya ubunifu.


Amesema kuwa, baraza limefanya maamuzi ya kuwachagua Ritha Paulsen (Madam Ritha) na Mrisho Mpoto (Mjomba) kuwa Mabalozi watakaofanya kazi kuhakikisha wanalitangaza baraza kwa wadau wao ili wafahamu falsafa ya utekelezaji wa shughuli zao.


Aidha, amesema kwa mujibu wa mtiririko wa utekelezaji wa shughuli za sanaa nchini baraza limedhamiria kuwa na mabalozi watakaofanya kazi ya kulitangaza na kuwa wawakilishi wa baraza katika kutekeleza majukumu yake ndani na nje ya nchi ili kuitambulisha kuwa ni taasisi inayoshughulikia mustakabali wa maendeleo ya wasanii na wadau wa sanaa nchini.


"Ushirikiano huu wa baraza na mabalozi umejikita katika makubaliano ya kufanya kazi kwa muda wa miezi 12 kuanzia leo ambapo tutasaini mkataba wa maridhiano"amesema Dkt. Mapana.



Akizungumza mara baada ya kusaini mkataba huo Ritha Paulsen amesema kuwa atahakikisha anafanya kazi kwa mujibu wa mkataba huo na kujitolea kwa moyo wote kuhakikisha malengo ya baraza hilo linafikiwa kama ambavyo wamekubaliana.


Aidha, amesema wamelihakikishia Baraza kuwa wanao uwezo wa kuifanya kazi hiyo kwa kupitia ushawishi na uzoefu walio nao kwenye tasnia ya sanaa hivyo wadau wao wakae tayari kwa mambo mazuri yajayo.


Ametaja maeneo ya msingi ambayo watashughulika nayo kwenye kulitangaza baraza kuwa ni pamoja na kutumia vyombo vya habari au mitandao ya kijamii kutangaza shughuli za Baraza pamoja na kushiriki katika warsha au matukio mbalimbali ya Sanaa ambapo watatumia majukwaa hayo kuwafikia wadau na kulitangaza baraza.



Katika hatua nyingine BASATA kwa kushirikiana na Taasisi ya "Music in Africa Foundation wanatarajia kufanya tamasha la ACCES ambalo litafanyika hapa nchini Novemba 9-11, mwaka huu kwa mara ya pili ambapo litawashirikisha wasanii wote nchini wakiwemo chipukizi na waliofanikiwa katika uga wa muziki.


Aidha, lengo la tamasha hilo ambalo linandaliwa na Taasisi ya Music in Africa kwa kushirikiana na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ya Tanzania ni kuwasaidia wanamuziki kutambuana na kuonyesha uwezo wao wa kuimba pamoja nakufundishwa namna ya kuchangamkia fursa za masoko ya ndani na nje ya nchi.


Aidha, tamasha hilo la ACCES linatarajiwa kuhudhuriwa na wadau wa muziki zaidi ya 1000 kutoka zaidi ya mataifa 50 duniani ambapo kwa Tanzania linafanyika kwa mara ya pili ambapo mwaka jana lilifanyika Novemba 24-26, 2022 jijini Dar es Salaam.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI