Header Ads Widget

VIONGOZI WA VYAMA VYA UPINZANI WAONYWA KUICHEZEA AMANI ILIYOPO.

 



Na Mbaruku Yusuph,Matukio Daima APP Tanga .


VIONGOZI wa vyama vya siasa toka upinzani Mkoani Tanga wametakiwa kuacha kuichezea amani na utulivu uliyopo na watambue kufanya hivyo ni kuhatarisha usalama wa Taifa kwa ujumla.


Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi mkoa wa Tanga Rajabu Abdurahman wakati akiwahutubia wananchi wa kata ya Msambweni Mkoani hapa na kusema wananchi wanapaswa kuilinda tunu ya amani iliyopo.


Rajabu ambae pia ni Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa wa chama hicho alisema vipo viashiria vya wazi kwa vyama hivyo vya upinzani kuhusiana na uvunjifu wa amani hasa pale wanapofanya mikutano yao ya hadhara na kudhihaki viongozi wa ccm na Serikali.


Aidha alisema Mh,Rais Dk Samia Suluhu Hassan anatumia busara kubwa kuilinda amani iliyopo kwa Watanzania tofauti na vyama vya upinzani ambavyo vinajaribu kutumia nguvu kuivuruga jambo ambalo halitapewa nafasi.


"Wasitumie majukwaa ya kisiasa kupandikiza chuki za ubaguzi wa kidini na nawaasa ndugu zangu tuwapuuze na sera zao za kibaguzi ambazo hazina mwisho mwema kwa Taifa na Mkoa wetu"Alisema Rajabu.


Alisema kutokana na vyama hivyo kukosa sera na hoja za kuzungumza mbele ya wanachama wao na Watanzania kwa ujumla,mikutano yao imekuwa na agenda moja ya kuwapotosha wananchi juu ya mchakato wa uwekazaji wa bandari ya Dar es salaam dhidi ya Kampuni ya Dubai Ports World (DP WORLD).


Alisema agenda ya bandari ndio imekuwa ikizungumzwa na vyama vya upinzani hasakipindi hiki cha kuelekea kwenye chaguzi za Serikali na mitaa 2024 na uchaguzi Mkuu 2025 jambo ambalo halitapewa nafasi Mkoani hapa.


Rajabu alisema Serikali ya CCM ipo makini na inayo mpango mahususi wa kutaka kuifanya Bandari hiyo kuwa lango kuu la kiuchumi kwa maslahi ya Taifa tofauti na inavyotafsiriwa na wapinzani ya kuwa bandari hiyo imeuzwa kwa Taifa hilo la Kiarabu.


Mbali na hayo pia Mwenyekiti huyo aliwaambia wananchi katika Mkutano huo kuwa ndani ya miezi sita Serikali imetoa Bil 356.8 kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo Elimu,Afya,miundombinu,na maji.


Alisema ipo miradi mkakati ya kuufungua Mkoa wa Tanga na tayari Serikali imetoa fedha za kutosha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Tanga,Pangani, Saadan hadi Bagamoyo kuelekea Jijini Dar es Salaam sambamba na ujenzi wa daraja katika mto Pangani lenye urefu wa mita 525 na wakandarasi wapo site sambamba na mradi wa ujenzi wa barabara toka Handeni,kibrashi,Kilindi hadi kiteto.


Mbali na mradi huo pia Serikali ilitoa Shs Bil 429 kwa ajili ya utanuzi wa Bandari ya Tanga na maboresho ya gati moja ambapo tayari meli kubwa zimeanza kutia nanga gatini tofauti na hapo awali ambapo bandari hiyo haikuwa na uwezo kwa kuhudumia meli kubwa.


Hata hivyo aliwaomba wananchi Mkoani hapa kuwa wanahakikisha wanamuunga mkono Rais Samia Suluhu katika jitihada zake za utekelezaji wa miradi mkakati ya kimaendeleo ambayo yote ipo katika ilani ya chama hicho ya mwaka 2020/2025.




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI