Header Ads Widget

WANANCHI WATAKIWA KUTUNZA MIRADI INAYOJENGWA NA SERIKALI.



NA WILLIUM PAUL, SAME.

CHAMA cha Mapinduzi mkoa wa Kilimanjaro kimewataka wananchi kuilinda miradi inayotekelezwa na Serikali ili iweze kuwanufaisha kwa muda mrefu na kufikia lengo lililokusudiwa.



Kauli hiyo ilitolewa na Katibu wa CCM mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya wakati wa ziara ya Kamati ya siasa mkoa kukagua miradi ya barabara, Afya na Elimu katika wilaya ya Same ikiwa ni ukaguzi wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020.



Mabihya alisema kuwa, Serikali ya awamu ya sita inawajali na kuwapenda wananchi na kuwataka kutembea kifua mbele huku wakitambua miradi hiyo ni mali yao hivyo wanawajibu wa kuilinda.


Akiwa katika ukaguzi wa daraja la Kalemawe kata ya Kalemawe Jimbo la Same mashariki lenye urefu wa mita 36, Kamati hiyo ya siasa iliwaonya wananchi kuacha tabia kuchimba mchanga pembezoni mwa barabara pamoja na Madaraja kwani kufanya hivyo kunapelekea miundombinu kushindwa kudumu muda mrefu.



"Baada ya kuteseka kwa muda mrefu kwa kukosa kivuko na kupelekea vifo vya wananchi wakiwamo wakinamama wajawazito na wagonjwa kwa kukosa kivuko hatimaye leo Serikali imewajengea daraja hili la kisasa sasa ni wajibu wenu kuhakikisha mnalilinda ili lidumu muda mrefu" alisema Mabihya.


Awali akisoma taarifa za ujenzi wa Daraja hilo kwa wajumbe wa Kamati ya siasa mkoa, Meneja wa Wakala wa barabara vijijini (Tarura) wilaya ya Same, Mhandisi James Mnene alisema kuwa, ujenzi wa daraja hilo kwa kutumia Teknolojia ya mawe uliibuliwa baada ya wananchi wa vijiji vya Makokane, Karamba, Mgandu, na Kalemawe kukumbana na adha ya muda mrefu ya kukosa kivuko.



Mhandisi Mnene alisema kuwa, ujenzi wa daraja hilo pamoja na uchongaji wa barabara kwa urefu wa kilomita 3.5 na kuweka changarawe umeigharimu Serikali milioni 376.277 na mradi upo katika hatua za mwisho kukamilika.


Kwa upande wao wananchi wa kata hiyo ya Kalemawe waliwaeleza wajumbe wa Kamati ya siasa ya Chama cha Mapinduzi mkoa, kipindi cha mvua ambapo imekuwa ikipelekea maji mengi wamekuwa wakikosa mawasilia ya kutoka katika vijiji vyao kwa kukosa kivuko.



Amina Gadi mkazi wa kijiji cha Makokane alisema kuwa, kutokana na kukosekana kwa kivuko hicho kumelekea vifo kwa wakinamama wajawazito pamoja na wagonjwa kutokana na kushindwa kuvuka kipindi cha mvua kwenda hospitali kupata huduma.


"Kujengwa kwa daraja hili limeleta faraja kubwa kwa sisi wananchi wa Kalemawe na kufurahia maisha yetu tunamshukuru sana Rais Dkt Samia Suluhu Hasani na Serikali yake kwa kuona hili na tunamuahidi kumuunga mkono" alisema Amina.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI