Header Ads Widget

UJENZI WA BARABARA YA SAME-KISIWANI-MKOMAZI KWA KIWANGO CHA LAMI KUFUNGUA MAENDELEO YA WANANCHI WA SAME.

 


NA WILLIUM PAUL, SAME.


WANANCHI wa Tarafa za Gonja, Ndungu na Bendera wilayani Same mkoani Kilimanjaro ambao ni wakulima wakubwa wa mazao ya biashara kama Tangawizi wanatarajia kunufaika na biashara hiyo baada ya Serikali kuwajengea mazingira rafiki ya kufikisha mazao yao sokoni kwa kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Same-Kisiwani-Mkomazi.


Hayo yalibainishwa na Mkuu wa kitengo cha matengenezo ya barabara Tanroad mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Benitho Nikodemu wakati wa ziara ya Wajumbe wa Kamati ya siasa ya Chama cha Mapinduzi mkoa wa Kilimanjaro walipotembelea barabara hiyo kujionea ujenzi wa kilomita 5.2 kwa kiwango cha lami.



Mhandisi Nikodemu alisema kuwa, mikakati ya Serikali ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii wilaya ya Same ni pamoja na kuboresha mtandao wa barabara ili kuongeza ufanisi katika sekta ya usafirishaji.


Alisema kuwa, ujenzi wa kilomita hizo 5.2 utaigharimu Serikali Bilioni 6.330 ambapo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/23 Serikali imeamua kujenga barabara yote iliyobaki yenye urefu wa kilomita 92.8.



Mhandisi huyo alisema kuwa, mradi umefikia asilimia 45, na changamoto ambazo wamekuwa wakikutana nazo mi kuongezeka kwa kazi eneo la tindiga ambapo baada ya kazi ya usanifu pembezoni na kuchimba ilibainika eneo kubwa lina udongo usiofaa na ongezeko la chemichemi.


Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya alisema kuwa, aliwaomba Wakala wa barabara nchini Tanroad mkoa wa Kilimanjaro pamoja na Wakandari wa ujenzi wa barabara hiyo kuhakikisha thamani ya fedha iendane na kazi ili barabara hiyo iweze kudumu muda mrefu.


Mabihya alisema kuwa, ubora wa barabara hiyo itasaidia kutekeleza miradi mingine la kuwataka wakandara kujenga Imani kwa Serikali ili waweze kupata kazi nyingine.


"Wakandari mnapaswa kutambua kujenga kwenu barabara hii kwa kiwango kinachostahi ndivyo mtakavyojitangaza kwa Serikali na kuweza kupata kazi nyingi sasa sisi kama CCM hatutegemei barabara hii kujengwa chini ya kiwango" alisema Mabihya.


Alisema kuwa, kukamilika kwa barabara hiyo kutapunguza gharama za wananchi kusafirisha mazao yao kufika sokoni pamoja na kupunguza muda wa kusafiri.


Aidha Katibu huyo alidai kuwa pia kufunguka kwa barabara hiyo kutaongeza chachu ya kufungua mbuga ya wanyama ya Mkomazi na kuongeza kipato kwa Serikali pamoja na wananchi wake.

Mwisho..

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI