Header Ads Widget

SERIKALI YAWEKA MAZINGIRA WEZESHI YA MIKOPO KWA WACHIMBAJI WADOGO

 



Na Fadhili Abdallah,Kigoma


TUME ya madini imesema kuwa serikali imeweka mazingira mazuri yatakayowawezesha wachimbaji wadogo kupata mikopo kutoka taasisi za fedha ili kuzifanya shughuli zao kuwa na tija lakini kupunguza ajali migodini.

 

Mkaguzi wa migodi na mazingira wa tume hiyo, Mhandisi Henry Mditi alisema hayo akifunga mafunzo ya siku mbili kwa wachimbaji wadogo wa mkoa Kigoma kuhusu uchimbaji salama na wenye tija na kubainisha kuwa serikali imeondoa masharti magumu kwa taasisi za fedha ili wachimbaji waweze kupata mikopo.


Mditi alisema kuwa awali kulikuwa na shida kubwa kwa wachimbaji wadogo kupata mikopo kwenye taasisi za fedha kutokana na kutokuwa na dhamana zinazozishawishi benki kutoa mikopo lakini pia wachimbaji hawakuwa na vyama vinavyoeleweka.

 

“Kwa sasa serikali imeongea na mabenki na kuwa mdhamini wa wachimbaji wadogo kwa baadhi ya masharti ya mikopo kuondolewa na hiyo itawawezesha wachimbaji kuweza kukopa na kununua vifaa vya kisasa vya uchimbaji ambavyo vinatija kubwa katika kupunguza ajali migodini,” Alisema Mhandisi huyo.



Akizungumzia hali hiyo Katibu Msaidizi wa Chama cha wachimba madini mkoa Kigoma (KIGOREMA),Boaz  Mkohozi alisema kuwa kwa sasa mabenki yamepunguza masharti ili kuruhusu wachimbaji wadogo waweze kupata mikopo ukilinganisha na masharti magumu yaliyokuwepo awali ambayo yalikuwa kikwazo kwa wachimbaji wadogo kupata mikopo.


Hata hivyo Katibu huyo alisema kuwa kwa sasa wachimbaji wameelekeza nguvu zao kwa benki mpya ya wachimbaji inayoanzishwa ambapo wanaamini watapata mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya kuendelea shughuli zao.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI