NA WILLIUM PAUL, SAME.
KAMATI ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi mkoa wa Kilimanjaro imeridhishwa na shughuli ya ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Same unaoendelea na kuitaka Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Same kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi huo huo.
Kauli hiyo ilitolewa jana ikiwa ni mwendelezo wa kamati hiyo kukagua utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020 ambapo wamekagua miradi ya barabara, Afya na maji katika wilaya hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya Wajumbe wa Kamati ya siasa, Katibu wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya alisema kuwa, wameridhishwa na ujenzi ulipofikia na thamani ya fedha inaonekana.
"Yapo majengo yameshakamilika na thamani yake inaoneka hivyo tumeridhishwa na ujenzi hii lakini niwaombe watumishi msibweteke endeleeni kufanya kazi ya kuwasimamia mafundi ili mradi uendelee kuwa wa kiwango hiki hiki" alisema Mabihya.
Alisema kuwa, ili wananchi waweze kuzalisha mali na kukuza uchumi ni lazima Afya zao ziwe bora na Serikali ya Chama cha Mapinduzi haijabaki nyuma ndio maana imekuwa ikijenga hospitali kubwa na za kisiasa ili wananchi waweze kupata huduma karibu.
Alisema kuwa, chama cha Mapinduzi kilipita kwa wananchi kunadi Ilani yake hivyo wao wanapita kujionea ahadi zilizotolewa jinsi zinavyotekelezwa.
Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa hospitali hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Same, Anastazia Tutuba alisema kuwa, mradi wa ujenzi huo uliibuliwa kwa ajili ya kuboresha huduma za Afya kwa wananchi wa wilaya ya same kutokana na hospitali iliyopo kuwa chakavu pamoja na ufinyu wa miundombinu.
Alisema kuwa, mradi huo unatekelezwa ikiwa ni ahadi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hasani katika kampeni za mwaka 2020 ambapo unatekelezwa kwa awamu kulingana na mapokeo ya fedha.
"Hospitali hii mpaka kukamilika kwake utaigharimu Serikali Bilioni 7 na mradi huu unatekelezwa kwa kutumia fosi akaunti kwa kutumia mafundi wazawa" alisema Anastazia.
Aliendelea kudai kuwa, katika awamu ya kwanza ilikuwa ni ujenzi wa Majengo matano ambayo ni wagonjwa wa nje, jengo la kujifadhia dawa, jengo la maabara, jengo la mionzi pamoja na jengo la mama na mtoto ambapo kwa sasa majengo hayo yapo katika hatua za mwisho za ukamilishaji.
Aidha alisema kuwa, pindi majengo hayo yatakapokamilika yataanza kutoa huduma kwa wananchi lengo likiwa ni kufikia lengo lililokusudiwa na Serikali.
Mwisho..
0 Comments