Header Ads Widget

FICHUA WAKWEPA KODI 'ULAMBE' ASILIMIA TATU

 

Mkurugenzi wa wa Huduma na Elimu  ya Mlipa kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),Richard Kayombo, akizungumza wakati wa semina kwa waandishi wa habari wa Klabu ya Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC) kuhusu ya masuala mbalimbali ya kikodi na umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo ya taifa, semina hiyo imefanyika leo.
Washiriki wa Semina ya elimu kwa mlipa kodi wakiwa katika picha ya pamoja na maofisa wa Mamlaka ya Mapata Tanzanzia TRA.
Ofisa Mkuu wa Usimamizi wa Kodi wa TRA, Hamad Mterry, akiwasilisha mada kuhusu majukumu ya msingi yanayosimamiwa na mamlaka ya TRA ya kukadiria, kukusanya na kuhasibu mapato ya serikali kuu kwa mujibu wa sheria zilizowekwa wakati wa semina kwa wanahabari wa Klabu ya Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC) leo.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

NA ARODIA PETER, MATUKIODAIMA App, Dar

MOJA ya vitu ambavyo Watanzania walio wengi hawavifahamu ni namna wanavyoweza kufaidika na hata kutajirika kwa kuwaripoti kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) watu au kampuni zinazokwepa kodi nchini.


Hayo yamebainishwa na Afisa Mkuu wa Usimamizi wa Kodi wa TRA, Hamad Idd Mterry wakati wa semina kwa Klabu ya waandishi wa habari wa Jiji la Dar es Salaam iliyohusu Elimu kuhusu kodi iliyofanyika Juni 6, 2023.


Mterry alisema ili kuhakikisha kodi ya Serikali inatozwa pasipokuacha mianya ya ukwepaji, Mamlaka hiyo inayo sheria ya kutoa kamisheni ya asilimia tatu ya kodi iliyokwepwa kwa mtu atakayetoa taarifa sahihi kwa TRA.


"Utaratibu huo upo kisheria, mtu yeyote atakayetoa taarifa sahihi za mkwepa kodi basi atajizolea asilimia tatu ya kodi iliyokwepwa na muhusika. 

Hivyo nitoe wito kwa wananchi kwamba kuna dili la namna hiyo, wengine wanatajirika kwa wao kutuletea taarifa sahihi na sisi tukazifanyia kazi na kujiridhisha basi wanachukua hiyo kamisheni." alisema Mterry.

 Aidha Mkuu huyo wa Usimamizi wa Kodi wa TRA alizungumzia suala la kila Mtanzania mwenye umri kuanzia miaka 18 kuwa na Namba ya mlipa kodi (TIN).


Alisema mabadiliko ya Sheria ya mwaka 2022 yameweka ukomo kwamba ifikapo Desemba mwaka huu 2023 kila Mtanzania atapaswa kuwa na TIN.


Kwa wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama Wamachinga ni lazima kuwa na namba hiyo na ikiwa mtaji wake hauzidi Shilingi milioni 4 basi hawezi kutozwa kodi ya mapato.


Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo kwa upande wake aliwasihi waandishi wa habari kuwa mabalozi wazuri katika kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa ulipaji kodi nchini.


Alisema lengo la semina hiyo ni kukumbushana kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu kodi ili kila Mtanzania ajione anao wajibu wa kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa lake.


"Sisi TRA tunayo kauli mbiu yetu inayosema Kwa pamoja tunajenga Taifa letu, hivyo tuikumbushe jamii kwamba maendeleo haya wanayoyaona ni matokeo ya kodi zinazokusanywa na TRA.


"Wote tukitambua ukweli huo kwamba hii miundombinu tunayoiona, ulinzi, huduma mbalimbali hospitalini vyote hivi vinatokana na kodi tunayokusanya kutoka kwao Watanzania, hivyo watuunge mkono kwa kulipa kodi stahiki"alisisitiza mkurugenzi huyo na kuongeza kuwa.


"TRA inaendelea kufanya jitihada zaidi kuhakikisha udanganyifu wowote katika mashine za kielektroniki unakomeshwa kabisa.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI