Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MAMLAKA ya mapato Tanzania (TRA) Mkoani Kigoma imeeleza kuwa licha ya utoaji wa elimu ya mlipa kodi kwa jamii bado kumekuwa na changamoto ya utoaji risiti hasa maeneo ya vijijini ambapo kumekuwa kukifanyika shughuli za kibiashara ikiwemo kilimo.
Hayo yamebainishwa na meneja wa TRA Mkoani hapa DEOGRATIUS SHUMA katika kampeni ya TUWAJIBIKE iliyolenga kutoa elimu kwa wafanya biashara katika zoezi la ununuzi na utoaji wa risiti kwa kila bidhaa.
Shuma amesema kwa miaka ya karibuni kumekuwa na mabadiliko ya ongezeko la kutoa na kudai risiti lakini bado limekuwa halijitoshelezi kulingana na uwepo wa biashara ambazo zinatambulika na mamlaka hiyo.
Katika zoezi hilo baadhi ya wafanyabiashara waliopo katika taasisi za elimu akiwemo Starkisha Nyaga Mkuu wa shule ya msingi Shabbir ambaye ameeleza kuwa kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa risiti hasa katika manunuzi ya bidhaa za nafaka kutoka maeneo ya vijijini.
Naye Martha Michael, Mhasibu kutoka Sunset Vista Hotel ya Mjini Kigoma alisema kuwa wanapata shida kupata risiti za EFD wanapofanya manunuzi ya bidhaa za vyakula na viungo katika masoko mbalimbali ya mkoa Kigoma.
Akizungumzia kampeni hiyo Katibu tawala msaidizi seksheni ya uchumi ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kigoma, Ntime Mwalyambi alisema kuwa zoezi hilo la kuhamsisha kutoa na kudai risiti ni muhimu kwa wafanyabiashara kuunga mkono juhudi za ukusanyaji wa mapato kwa kutumia mashine za EFD ili kuongeza pato la Taifa litakalo wezesha kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara.
Kampeni ya TUWAJIBIKE ilizinduliwa Machi 2 mwaka huu ikiwa na malengo ya kutoa risiti halali,kudai risiti halali na kuchukua hatua kwa wauzaji wasitoa risiti halali za EFD.
0 Comments