Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Takribani wanafunzi 800 wa shule ya sekondari ya wasichana Manyunyu iliyopo Matembwe katika halmashauri ya wilaya ya Njombe wamepatiwa Taulo za kike ili kuwalinda pindi wanapokuwa katika kipindi cha hedhi.
Taulo hizo za kike zimetolewa na taasisi ya Flaviana Matata ambapo Afisa miradi wa taasisi hiyo Bi.Suzan Cleopas amesema utoaji wa pedi hizo umeambatana na elimu ya hedhi salama.
Mkurugenzi Mtendajiwa wa Taasisi hiyo na Lavy Pads Flaviana Matata ambaye ni Mwanamitindo amesema kwa kushirikiana na wizara ya elimu na wadau wengine wataboresha miundombinu ya maji, vyoo na sehemu ya kuchomea (Pedi) zilizotumika katika maeneo ya shule ili kuwa na mazingira rafiki kwa wanafunzi wa kike na kufikia lengo la hedhi salama kwa wote.
Ameongeza kuwa bado kuna changamoto kwa baadhi ya jamii kuhisi hedhi ni jambo la aibu hivyo ni wakati wa kutoa elimu ili wanawake waone hedhi ni tunu na heshima.
Afisa Elimu ya Sekondari Halmashauri ya Wilaya ya Njombe CHARLES MESHACK na Twumwimbile Lufunyo Ndelwa ambaye ni Afisa Elimu ya Watu Wazima Idara ya Elimu Sekondari katika halmashauri hiyo wamesema pedi na elimu waliyoipata wanafunzi wana amini itawasaidia kijitambua,kuongeza ufaulu na kujiamini.
Makamu Mkuu Wa Shule ya Sekondari ya Manyunyu Noel Mtweve amekiri kuwapo kwa changamoto ya miundombinu ya vyoo na maji hasa katika shule zilizopo vijijini hivyo anapongeza kwa hatua ya Taasisi ya Flaviana Matata kuzipa kipaumbele shule za pembezoni mwa mji.
Nao baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari ya wasichana Manyunyu akiwemo Revina Mlowe na Mariam Komeka wamekiri kuwapo kwa adha ya upatikanaji wa taulo za kike kulingana na hali za kiuchumi kwa baadhi yao na hivyo wameishukuru taasisi ya Flaviana Matata.
Uongozi wa Taasisi hiyo umetembelea katika shule ya sekondari ya wasichana Manyunyu ikiwa ni mwendelezo wa maadhimisho ya hedhi salama.
0 Comments