Header Ads Widget

TATIZO LA SHINIKIZO LA JUU LA DAMU NI KUBWA TANZANIA




 Na Hamida Ramadhan Matukio Daima APP Dodoma.


WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu Amesema Tanzania tatizo la ugonjwa wa shinikizo la juu la damu ni kubwa ambapo kwa wagonjwa waliotibiwa katika Taasisi ya moyo Jakaya Kikwete (JKCI)tangu ilipoanzishwa Sept 2015 hadi April 2023 kati ya wagonjwa 619,102 waliotibiwa asilimia 66 kati yao walikuwa na shinikizo la juu la damu.


Waziri huyo ameyasema hayo leo jijini Dodoma kwenye maadhimisho ya siku ya Shinikizo la Juu la Damu Duniani ambapo amesema

Hali hiyo inamaanisha kuwa kwa kila wagonjwa 10 wanaoumwa hospitalini hapo, wagonjwa 6 wana ugonjwa wa shinikizo la damu.



Amesema katika uchunguzi uliofanywa katika jamii kwenye mikoa ya Pwani, Arusha,Geita, Mtwara,Lindi, Zanzibar,Iringa na Dar Es Salaam takwimu zinaonesha watu 3 hadi 4 kati ya 10 wana shinikizo la damu la juu .


Amesema Shinikizo la juu la damu ndio sababu kubwa ya kiharusi,shambulio la moyo,moyo kushindwa kufanya kazi,kutuna kwa kuta za mishipa ya damu ,moyo,uharibifu kwenye chujio za Figo,ganzi miguuni na mikononi,upofu na kupunguza nguvu za kiume.


"Takwimu za Tanzania kutoka mfumo wa ukusanyaji taarifa za afya zinaonesha kuwa jumla ya wagonjwa 2,535,281 walitibiwa magonjwa yasiyoambukizwa kwenye vituo vya afya kwa mwaka 2017," Amesema Waziri Ummy


Ameeleza kuwa wagonjwa hao wameongezeka hadi kufikia wagonjwa 3,440,708 Kwa mwaka 2021 ambapo ongezeko hilo wako wagonjwa 905,427 Kwa kipindi cha miaka mitano ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 9.4.



Amesema  wagonjwa wa shinikizo la juu la damu ndio ulioongoza miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza ambapo waliongezeka Kutoka wagonjwa 688,901 Kwa mwaka 2017,hadi kufikia wagonjwa 1,345,847 kwa mwaka sawa na ongezeko la asilimia 95.4 katika kipindi hicho.


"Kwa takwimu hizo inaonyesha kwamba wagonjwa Wenye shinikizo la damu wameongezeka takribani mara mbili zaidi Kwa kipindi cha miaka mitano,"amesema Waziri Ummy 


Kutokana na hayo Waziri Ummy amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa Sera ya afya ya mwaka 2007 ambayo inalenga kutoa huduma kwa magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo shinikizo la damu Kwa umahiri zaidi.


Ameeleza kuwa mpango wa Serikali kupitia Wizara hiyo ni kutoa mafunzo ya utoaji huduma za magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo shinikizo la damu Kwa watoa huduma 2400 kutoka vituo vya afya vyote 600 Katika mikoa 26 ambayo ni sawa na asilimia 73.



Kwa upande wake Prof. Pasco lubajo Mkurugenzi wa kinga Wizara ya afya ametumia nafasi hiyo kuhimiza wananchi kubadili mtindo wa maisha Kwa kufanya mazoezi, kuepuka tabia bwete, kupunguza ulevi, matumizi ya tumbaku na bidhaa zake na kuzingatia ulaji unaofaa.


Amesema jamii inapaswa kupunguza matumizi ya chumvi,sukari na vyakula vyenye mafuta mengi pamoja na kuzingatia unywaji wa maji ya kutosha angalau kiasi cha Lita 1.5 ya maji Kila siku.



Prof.Lubajo ameutaja ugonjwa wa shinikizo la juu la damu kuwa unasababishwa na nguvu ya msukumo wa damu Katika mishipa kuwa kubwa kuliko kawaida Kwa muda mrefu ambapo ongezeko hilo huulazimu moyo kufanya kazi kupita kiasi.





Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI