Header Ads Widget

NEEMA YAJA KWA WAKULIMA WA SKIMU ZA ASILI JIMBO LA MOSHI VIJIJINI, HAI NA VUNJO.

 


NA WILLIUM PAUL.

WANANCHI wa Jimbo la Moshi vijijini, Hai na Vunjo wanaotumia skimu za umwagiliaji za asili wanaenda kuondokana na tatizo la ubovu wa skimu hizo baada ya Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kutuma wakandari kukarabati na kujenga mifereji yote ya asili.

Hatua hiyo imekuja baada ya Mbunge wa Jimbo la Moshi vijijini, Prof Patrick Ndakidemi kuhoji swali Bungeni, pamoja na  Serikali kutoa miche bora ya kahawa bure, je Serikali ina mikakati gani kuboresha Skimu za asili za umwagiliaji ili wakulima wapate maji ya kumwagilia kwani miche bora bila maji hatutaongeza tija.


Mbunge huyo aliuliza pia je Serikali ina mkakati gani wa kusindika kahawa aina ya Arabika kwa sababu kahawa hii ina soko nzuri sana katika soko la dunia.


Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Kilimo, Antony Mavunde alisema kuwa, Wizara inayo wakandarasi ambapo katika mkoa wa Kilimanjaro wanaotekeleza miradi ya umwagiliaji na wameshawapa maelekezo watakwenda kukarabati na kujenga mifereji yote ya asili inayogusa jimbo la Moshi vijijini, Hai na Vunjo.


Mavunde alisema kuwa, pia Serikali inayomkakati wa dhati wa kuhakikisha kahawa itaendelea kusindikwa na isiuzwe ambayo haijasindikwa ambapo bodi ya kawaha imeshatoa zaidi ya leseni 20 kwa ajili ya wasindikaji ili kuchochea usindikaji wa zao la kahawa na kutengeneza masoko ya uhakika ambapo kwa sasa kahawa inauzwa kwa wingi nchini Japan.


Aidha Mbunge Prof Ndakidemi alihoji je Serikali ina mpango gani wa kuwapa wakulima wa KAHAWA ruzuku ya kununua dawa za kahawa kama ilivyokuwa awali. 


Naibu Waziri akijibu swali hilo alisema kuwa, matumizi ya viwatilifu katika zao la kahawa ni njia ya uthibiti wa visumbufu vya zao la kahawa ili kulinda ubora wa mazao yanayozalishwa dhidi ya magonjwa ya kutu ya majani na cholebuni.


Alisema kuwa, utafiti wa zao la kahawa umebaini kuwa upandaji wa miche bora ya kahawa ni njia pekee inayowezesha kuzalisha mazao yenye tija nzuri ukinzani dhidi ya wadudu waharibifu na magonjwa ya zao la kahawa na kupunguza matumizi ya viwatilifu kwa kahawa kwa asilimia 40.


"Kwa sasa Serikali haina utaratibu wa kutoa ruzuku ya viwatilifu vya kahawa bali kupitia taasisi ya utafiti wa kahawa Tacri na Bodi ya kahawa nchini (TCB) zimeendelea kuzalisha, kusambaza na kuhamasisha wakulima kubadilisha mikahawa ya zamani kwa kupanda miche mipya ambayo inaukinzani dhidi ya magonjwa" alisema Naibu Waziri Mavunde.

Alisema kuwa kwa mwaka 2019/2020 hadi 2021/2022 jumla ya miche zaidi ya milioni 41 imezalishwa na kugaiwa bure kwa wakulima.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI