Header Ads Widget

MBUNGE WA JIMBO LA MOSHI VIJIJINI ACHANGIA BAJETI YA WIZARA YA KILIMO

 


Na WILLIUM PAUL.

Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi ameishauri Serikali kuongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo kufikia trilioni 2 ili Wizara hiyo iweze kufanya kazi kwa uhakika na kufikia matakwa ya wakulima.


Prof. Ndakidemi alitoa kauli hiyo alipochangia bajeti ya Kilimo ambapo aliishukuru Serikali kwa kuiongoza bajeti Wizara hiyo kutoka Bilioni 954 mwaka wa fedha 2022/2023 mpaka kufikia Bilioni 970 kwenye bajeti ya mwaka 2023/2024.

Alisema kuwa, wakulima ndio sehemu kubwa ya uchumi na kama watawezeshwa wataonyesha maajabu makubwa katika kukuza uchumi.

"Kila Mbunge tumezaliwa na wakulima na hata kama hujazaliwa na mkulima basi tunakula chakula kinacholimwa na mkulima hivyo hii bajeti ni yetu sisi wakulima tunapaswa kuipitisha kwa kishindo ili iende kuwanufaisha wakulima" alisema Prof. Ndakidemi.

Alisema kuwa, fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya miradi ya Kilimo kwa mwaka 2023/2024 ni Bilioni 767 ambapo ni karibu asilimia 85 ya bajeti yote ya Kilimo.

Mbunge huyo alisema kuwa mradi wa ruzuku ya mbolea umeenda vizuri ambapo Bilioni 342 zimeshatumika na kuita Wizara ya Kilimo changamoto za usambazaji walizopitia kuzifanyia kazi kwani mwaka wa kwanza ulikuwa wa kujifunza na zoezi bado ni endelevu.

Akichangia upande wa Mbegu Mbunge huyo alisema kuwa, mbegu ndio msingi katika sekta ya Kilimo hivyo watafiti waongezewe fedha ya kutosha na ili kuwa na mbegu Bora ambazo zitaleta tija kwa wakulima.

"Ile sheria ya mbegu iboreshwe wapo watu wanazalisha mbegu za asili na ile sheria inawakataza watu kuuza mbegu ambazo hazijapitia kwenye mfumo rasmi hivyo hii sheria iboreshwe ili wale wanaozalisha mbegu za asili watakapokidhi vigezo mbegu hizo za asili ziwafikie wakulima" alisema Prof. Ndakidemi.

Aidha Mbunge ameiomba Wizara iangalie kwa makini swala la vyama vya ushirika kwani kuna matatizo makubwa ya vyama ushirika jimboni kwake.


Pia ameiomba Wizara ya Kilimo imsaidie kuboresha skimu  za asili za umwagiliaji jimboni kwake, na kuomba kata ya Arusha Chini ijengewe skimu mpya ya umwagiliaji katika eneo lenye hekta 2000.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI