Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Licha ya kuripotiwa kuwapo kwa ubabaishaji wa upatikanaji wa mbolea za ruzuku kwa Wakulima wa mazao ya chakula kwenye baadhi ya maeneo mkoani Njombe,lakini duru zimearifu kuwapo kwa mazao yanayotia moyo mashambani kutokana na mbolea zilizopatikana.
Aidha Uzalishaji shambani umeongezeka kwa kiasi kikubwa katika msimu huu wa kilimo, ikiwa ni matokeo chanya ya mpango wa serikali wa kuinua sekta ya kilimo kupitia Ruzuku kwenye pembejeo.
Baadhi ya wakulima akiwemo Nestory Mpika,Edda Sanga na Yohan Mhagama wamesema kwa sasa hali ya uzalishaji shambani inaridhisha tofauti na misimu kadhaa ya kilimo iliyopita, wakibainisha kuwa gharama ya pembejeo ndio ilikuwa kikwazo kwao cha kufikia uzalishaji wenye tija.
Hata hivyo wakulima wengine akiwemo Leonard Kisangani na Elbart Nyagenda wanaiomba serikali kuanza mchakato wa upatikanaji wa mbegu mbora pamoja na mchakato wa upelekaji mbolea karibu na maeneo ya wakulima mapema katika kuendelea kuboresha zaidi sekta ya kilimo katika msimu ujao.
Kikwazo kikubwa kwa wakulima katika msimu uliopita ni ucheleweshwaji wa upatikanaji wa mbolea ambapo baadhi ya mawakala mjini Makambako akiwemo Oraph Mhema wanasema tayari mzigo upo wa kutosha maghalani.
Uaminifu kwa mawakala wa mbolea unaendelea kusisitizwa na mkuu wa Idara ya kilimo Makambako Beatrice Tarimo huku mbunge wa Ludewa Joseph Kamonga akiomba kuongezwa kwa maghala ya chakula wilayani kwake.
Tayari Wizara ya Kilimo chini ya waziri wake Hussein Bashe imefanikiwa kupitisha bungeni bajeti ya shilingi bilioni 970,785,619,000 kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024 ikiwa ni ongezeko la asilimia 29.24 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka uliopita.
0 Comments