Header Ads Widget

MAKALA , MICHEZO NA ZANA ZA UJIFUNZAJI VINAVYOWEZA KUMSAIDIA MTOTO KATIKA UJIFUNZAJI WA AWALI

 





NA HADIJA OMARY LINDI


Imeelezwa kuwa, mtoto  mdogo anapojifunza kwa matendo kupitia michezo na zana mbalimbali  inampa nafasi ya kutumia milango ya fahamu na kupata utambuzi juu ya maswala kadhaa anayojifunza.


Hayo yamebainishwa na Afisa Elimu Awali na Msingi Halmashauri ya Ruangwa Mkoani Lindi Geoge Mbesigwe  alipokuwa akizungumza na Matukio Daima kwenye mahojiano maalumu, ilipotaka kujua namna michezo inavyoweza kumsaidia mtoto katika ujifunzaji wa elimu ya awali.


Alisema katika malezi na makuzi ya mtoto umri wa mpaka miaka nane (8)  katika kila anachojifunza kuhusu mazingira yake kinategemeana na aina ya michezo anayoshiriki.



Alisema hiyo ndio sababu ya walimu ngazi ya awali kwenye elimu msingi wanafundishwa mbinu za kubuni michezo ya aina mbalimbali ili kuwasaidia watoto kujifunza misingi ya kusoma kuandika na kuhesabu.


Hata hivyo, mwalimu Mbesigwe alieleza  ikiwa mazingira unayomuandalia mtoto ni ya elimu basi unapomfundisha utakuta darasani zimeandikwa namba ukutani kwa hivyo mwalimu anaweza kumfundisha mtoto wimbo wa kuhesabu lakini wakati huo huo anatamka na kuonyesha kwenye ukuta.



Alisema kupitia  matendo hayo ya kurudia rudia kupitia michezo mtoto pale pale akili yake inashika na anabadilika kutoka kwenye maisha ya kawaida ya anaingia kwenye maisha ya kujifunza .


Naye mwalimu wa darasa la Awali Shule ya Msingi Namakonde halmashauri ya Ruangwa ,  Madam Kambanga alisema kuwa ni muhimu kwa watoto wa madarasa ya awali kuanza kujifunza kwa kutumia zana au vifaa na michezo mbali mbali kabla ya kuanza kujifunza kwa kuandika na kalamu ya risasi kwenye Dafutari.



Aidha Madam Kambanga aliongeza kuwa hiyo ni kutokana katika kipindi hicho  ubongo wa mtoto unakuwa haujakomaa kusikiliza na kushika mambo mengi tofauti na watoto wengine wa madarasa ya juu, hivyo ni muhimu kuwafundisha kwa kutumia zana na michezo mbali mbali ili waweze kushika mambo kwa urahisi.


" Watoto wa madarasa haya wanapaswa kujifunza kwa kuona na kutenda wenyewe kwa kuwawekea vitu kwa ajili ya utambulisho wa vitu na matendo mbalimbali, hapo hapo watafurahi lakini pia watajifunza na hata kuwafanya wapende shule" .




Akizungumzia hali ya uandikishaji wa wanafunzi kwa madarasa ya awali na la kwanza ofisa elimu awali na msingi Halmashauri ya Ruangwa mwalimu George Mbesigwe alisema mpaka sasa Halmashauri hiyo wamevuka lengo la maoteo ya uandikishaji wa wanafunzi ambapo mpaka sasa wameshafika asilimia 117 % .


Alisema kwa mwaka wa masomo 2023 Halmashauri hiyo iliotea kuandikisha wanafunzi wa awali 3,367, wavulana 1,664 na wasichana 1,703 ambapo mpaka Februari  2, 2023 tayari wameshaandikisha wanafunzi 4087 ambapo wavulana ni 2068 na wasichana ni 2,019 sawa na asilimia 121%.


Kwa wanafunzi wa darasa la kwanza maoteo yalikuwa 3,403 wasichana 1,674 na wavulana 1,729 ambapo mpaka sasa tayari wameshaandikisha wanafunzi 3,471 wavulana 2,013 na wasichana1,958 sawa na asilimia 117%.


Mbesigwe alisema hali ya uandikishaji kwa mwaka 2023 imeongezeka mara dufu ukilinganisha na mwaka jana ambapo kwa mwezi kama huu wa Februari uandikishaji ulikuwa ni asilimia 75% kwa darasa la kwanza na asilimia 65% kwa awali.


Hata hivyo Mbesigwe alisema zipo sababu mbali mbali zilizopelekea uandikishaji wa wanafunzi hao kupanda ambazo ni pamoja na mabadiliko ya uandikishaji wa wanafunzi ambapo miaka ya nyuma uandikishaji huo ulikuwa ukifanyika kuanzia Disemba mpaka Machi na sasa unafanyika Oktoba mpaka Disemba



Kwa upande wake mtaalamu wa elimu ya awali Mwalimu Davis Gisuka kutoka shirika la Children in Crossfire,   lililojikita katika kutoa elimu  kwa walimu wa awali na kuwafundisha namna ya kuandaa madarasa  ya awali anasema, 


kama ilivyoweka wazi Sera ya Elimu na mafunzo ya mwaka 2014 ambayo inatumika hivi sasa kwamba lengo la elimu ya awali ni kumuandaa mtoto awe na utayari wa kuingia darasa la kwanza ambapo  utayari huo una maana ya kwamba mazingira ya ujifunzaji yamuandae mtoto kuwa tayari, lakini pia wazazi na walimu wajitume kwa ajili ya watoto.



“ Kikubwa zaidi ni namna gani mwalimu anaweza kuandaa darasa linalozungumza, na hii ndio sababu tunawafundisha walimu wacawalo kuwa na zana na michoro inayoendana na umri wa mtoto.



Zana zinaweza kuwa za kunig'iniza hewani kwa kutumia kamba au uzi, na Michoro ya ukutani” anaeleza mwalimu Davis Gisuka



"Vilevile, darasa la awali linapaswa kuwa na kona za ujifunzaji  ambazo ni maeneo yaliyowekwa vifaa/zana mbalimbali za kujifunzia  ambazo mtoto anaweza kujifunzia wakati wote kulingana na vionjo vyake"


 

Uandaaji wa kona za ujifunzaji hutegemea mahitaji ya  mtoto na ubunifu wa mwalimu kulingana na mazingira na umahiri unaotarajiwa  kujengwa na mtoto ndani au nje ya darasa. Kona hizi zinatakiwa kuwa na vifaa  vingi ambavyo vitamsaidia mtoto katika kutenda na kujifunza dhana mbalimbali.



“Idadi ya kona za ujifunzaji zinaweza kuwa pungufu au zaidi ya sita kulingana na ubunifu wake, mahitaji ya mtoto na mazingira yake ya ufundishaji na ujifunzaji.  Mwalimu anashauriwa kuhakikisha kwamba ana kona za lugha, hisabati na michezo.  Ni lazima ziandaliwe na zitumiwe na watoto,” Alifafanua Mwalimu Davis.


Kwa mujibu wa utekelezaji wa mtaala wa elimu ya awali, program ya mafunzo endelevu kwa mwalimu kazini moduli ya nne Taasisi ya Elimu Tanzania  mazingira rafiki ya kujifunzia ni jumla ya mambo yote yanayomzunguka mtoto. 


Mazingira hayo yanajumuisha darasa, choo na uwanja wa michezo ya nje. Ili Kuendeleza makuzi ya jumla kwa kila mtoto wa darasa la awali, mazingira ya Kujifunzia yanatakiwa yawe rafiki na ya kuvutia ili mtoto aweze kujifunza kwa urahisi.



Mwalimu anatakiwa awe mbunifu wa kuandaa mazingira rafiki ya kujifunzia yatakayoruhusu kila mtoto kujifunza kutokana na uwezo wake. Mazingira hayo ni lazima yawe ya kuvutia, safi, salama, yenye kuchochea ujifunzaji wa mtoto na yenye kuzingatia mahitaji ya kila mtoto wakiwamo wenye mahitaji maalumu.


Mtoto hujifunza kwa njia mbalimbali ikiwamo za uchunguzi, kugundua na kutatua matatizo. Hivyo, anapaswa apatiwe fursa ya kutumia vifaa akiwa peke yake au na watoto wengine katika kujifunza kupitia michezo na kona za ujifunzaji.


 


Hata hivyo kulingana na  muongozo wa Program Jumuishi ya Taifa ya Malezi Makuzi na Maendeleo ya Awali yam toto (PJT-MMMAM ) 2021/22 – 2025/26 ukurasa wa 19,   uwelewa juu ya umuhimu wa  ujifunzaji kupitia michezo  haukupewa kipaumbele katika ngazo zote za maamuzi , udhibiti ubora, watoa huduma , waelimishaji na jamii kwa ujumla ikiwemo wazazi.



Ambapo ripoti mbali mbali zinaonyesha kuwa matarajio makubwa ya wazazi ni mtoto wao kuanza kujifunza kusoma na kuandika katika madarasa ya awali  hivyo kupelekea watoa huduma kulazimika kuwafundisha watoto badala ya kuacha wajifunze kupitia michezo.



Programu hiyo pia inaonyesha mfumo wa elimu ya kuwaandaa walezi na walimu wa awali hauwaandai walimu katika falsafa ya ujifunzaji kupitia michezo katika umri mdogo. Hii inaendelea katika sekta zote zinazotoa afua za huduma ya awali pamoja na sekta binafsi.



Aidha kumekuwa na upungufu wa ujifunzaji wa watoto kupitia michezo wakiwa nyumbani na hata vituoni ambapo kwa upande mwingine kuna upungufu wa walezi wenye mafunzo ya elimu ya awali kukidhi ongezeko la program za elimu ya awali  huku ukubwa wa changamoto hiyo ikiwa ni vijijini ambako hakuna programu madhubuti za elimu ya malezi kabla ya watoto kujiunga elimu ya awali. 


Kwa upande wake Bashiru Kauchumbe mkazi wa Ruangwa alisema kuwa bado elimu inahitajika kwa wazazi kufahamu umuhimu wa michezo kwa watoto wao.



“Ni kweli kwa baadhi yetu sisi wazazi kuona watoto wanashiriki michezo wakiwa shuleni badala ya kukaa darasani kuandika tunaona sio sawa na huwenda tunaiona hiyo ni kupoteza muda na ndio maana tunaona kumpeleka mtoto kusoma darasa la awali ama chekechea ni kwa ajili ya mtoto kwenda kukua na sio kusoma”


Kupitia PJT-MMMAM serikali inashirikiana na wadau wanaotekeleza mradi wa Mtoto Kwanza, yaani Children in Crossfire, Mtandao wa Malezi Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto pamoja na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania kusambaza elimu ya malezi borakwa watoto wa Tanzania.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI