Header Ads Widget

KCB YAFADHILI VIJANA MASOMO YA UFUNDI.

 Na Jusline Marco : Arusha 

Benki ya KCB kwa kushirikiana na shirika la kijerumani la GIZ limetenga zaidi ya shilingi Bilioni mbili kwa ajili ya ufadhili wa vijana kwenye masomo ya ufundi Tanzania bara na visiwani kupitia mradi wa tujiajiri ambapo kwa mwaka huu wamelenga kuwalipia masomo vijana zaidi ya 5000.

Akizungumza katika mahafali ya vijana 146 yaliyofanyika VETA Oljoro, mkuu wa kitengo cha masoko,mahusiano na ustawi wa jamii Christine Manyenye amesema licha ya vijana hao kulipiwa mafunzo lakini pia waliofanya vizuri zaidi wamepewa vifaa vya kwenda kuanzia kazi.

"Mwaka huu tulipoonana na Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hasan, tulimwahidi kuwalipia vijana 5000 na wanatarajia kuanza masomo yao mwezi ujao" amesema Manyenya.

Kwa upande wake Mgeni rasmi katika maafali hayo ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela amesisitiza vijana hao kuweka malengo ya kujiajiri na kuajiri wengine.

"Naomba mtambue kuwa nyie ni mbegu iliyopandwa na inatakiwa kuota na kukua, vyeti hivi viwe mwanzo wa mafanikio" amesema Mongela.

Naye mmoja wa wanufaika Rogers Mbuguni waliopewa vitendea kazi kama vifaa vya ujenzi, useremala, upakaji rangi, uchomeleaji wameomba fursa hiyo iwafikie na vijana wengine.

"KCB na GiZ kama mlivyotushika mkono, tunaomba mwashike na wengine kwa sababu taifa hili linategemea nguvu za vijana na hawawezi kujikwamua kwani wengi wetu tunatoka familia duni" amesema Mbuguni.

Mradi wa tujiajiri ulioanza mwaka 2016, umekuwa ukiwezesha wanawake na vijana kupata mafunzo mbalimbali yanayowezesha kujiajiri kupitia vyuo vya ufundi vya Tanzania bara na visiwani.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI