Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP Njombe
Wizara ya mambo ya ndani imezindua kituo kipya cha polisi chenye ghorofa moja katika wilaya ya Wanging'ombe mkoani Njombe ikiwa ni moja ya usogezaji huduma karibu kwa wananchi.
Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoa wa Njombe Hamis Issah mpaka sasa ujenzi wa kituo hicho umegharimu shilingi milioni 948,388,951 zilizotolewa na serikali na kufanya kazi ya ujenzi kwa kutumia force akaunti.
Aidha kamanda Issah amesema licha ya kuwa tayari kwa matumizi kituo hicho lakini bado kinahitaji fedha kiasi cha shilingi milioni 240 kwa ajili ya uzio,samani na kibanda cha mlinzi ambavyo havikujumuishwa kwenye gharama za awali huku akisema bado kuna miradi mingine inaendelea kutekelezwa ukiwemo wa jengo lake.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa jeshi la polisi nchini IGP Camilius Wambura kamishna wa polisi idara ya fedha na Lojistiki nchini Liberatus Sabas amesema kwa mwaka 2021/2022 serikali ilitoa shilingi bilioni 2.5 zilizojenga majengo mbalimbali kikiwemo kituo hicho cha polisi.
Pia amesema kumekuwa na ongezeko la makosa makubwa katika kipindi cha mwaka huu kwani yameripotiwa makosa 40763 ya mauaji,ulawiti ujambazi wizi na ubakaji yanayosababishwa na migogoro ya ardhi,mapenzi,umasikini na tamaa za baadhi ya watanzania.
Hata hivyo katibu tawala mkoa wa Njombe Bi.Judica Omary kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Njombe amesema kujengwa kwa kituo kipya cha polisi daraja la kwanza katika wilaya ya Wanging'ombe ni moja ya jitihada za serikali kuendelea kuleta fedha ili kuwasaidia watanzania.
Akizungumza kabla ya kuzindua kituo hicho mgeni wa heshima katika tukio hilo Naibu Waziri wa mambo ya ndani Jumanne Sagini ameliagiza jeshi la polisi kuwaelimisha wananchi ili waendelee kuuchukia uhalifu na wahalifu kwani ongezeko la asilimia nne la makosa ukilinganisha na mwaka jana haliwezi kufumbiwa macho.
Wakazi wa wilaya ya Wanging'ombe akiwemo Gerod Kibumo,Danford Mpumilwa na Annamele Ngilangwa wanasema kujengwa kwa kituo hicho kunaweza kusaidia kupunguza matukio ya uhalifu na wahalifu yakiwemo mauaji.
Wilaya ya Wanging'ombe ni miongoni mwa wilaya za mkoa wa Njombe inayotajwa kuwa na idadi kubwa ya matukio na makosa mbalimbali yakiwemo mauaji ya kutisha.
0 Comments